Sakata la Asma Juma (29) anayedai kuibiwa pacha wake, limechukua sura mpya baada ya uongozi wa hospitali binafsi ya Huruma kusisitiza kuwa mtaalamu aliyechukua vipimo vya utrasound amekuwa akifanya kazi hiyo hata kwa mwajiri wake ambaye ni Serikali.
Kauli hiyo inapingana na iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Hopsitali ya Temeke, Amani Malima kwamba daktari aliyemfanyia Asma vipimo hivyo hana utaalamu huo na kwamba yeye kazi yake ni kupiga picha za x-ray na amekuwa akifanya vipimo vya ultrasound kama njia ya kumweka mjini.
Hospitali ya Temeke ndiyo inadaiwa na Asma kwamba imehusika na wizi wa mtoto wake mmoja baada ya ujauzito wake kuonyesha alikuwa na mapacha.
Lakini, jana Mganga Msimamizi wa Zahanati ya Huruma, Dk Erasmo Kuwendwa akiwa ameambatana na daktari aliyemfanyia mama huyo vipimo hivyo, alisema wana uhakika na vipimo vyao.
Dk Kuwendwa alisema kuwa mama huyo alifika katika zahanati hiyo na kufanya vipimo hivyo mara mbili na kwamba mara zote hizo alibainika ana mapacha na kwamba wote walikuwa na afya njema.
“Mara ya kwanza alifika hapa Februari 17 mwaka huu, alifanyiwa kipimo cha ultrasound na majibu yaliyoonekana ni kwamba ana mapacha ambao wote walikuwa salama na walikuwa na umri wa wiki 33.” alisema Dk Kuwendwa na kuongeza:
“Lakini pia Asma Juma alifika tena hapa Machi 7, mwaka huu, pia alifanyiwa kipimo hicho hicho na mtaalam wetu na kilichoonekana ni kwamba ana mapacha wenye umri wa wiki 36.”
Dk Kuwendwa alisema taarifa hizo ndizo zilizoko kwenye kumbukumbu zao na kwamba baada ya kufanyiwa vipimo hivyo mtaalam wao huwa anaandika ripoti na kisha anabandika na picha (image) za vipimo vya kile alichokiona.
Kuhusu taarifa za daktari aliyefanya vipimo hivyo kutokuwa na utaalam, Dk Kuwendwa alisema:
“Ninachojua mimi ni kwamba huyu mtaalam wetu aliyefanya hivyo vipimo ni mwajiriwa wa Serikali, ndani ya Manispaa ya Temeke, anafanya kazi Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, na huko anafanya x-ray, anafanya ultrasound na ni muda mrefu.”
Alisisitiza kuwa anaamini kuwa mtaalam huyo ana uzoefu na anajua kwamba ameajiriwa na Serikali kufanya kazi hizo hizo.
Alisema anashangaa kuwa picha za ‘ultrasound’ zimepotea na kusema kuwa hizo ndizo zingeleta majibu.
Wakati mkanganyiko huo ukitokea kamati iliyoundwa kuchunguza sakata hilo imemaliza kazi na kukabidhi ripoti kwa Mganga Mkuu wa Serikali, Mohamed Kambi.
Mganga Mkuu wa Hopsitali ya Temeke, Amani Malima jana alisema: “Tunasubiri tu majibu ya ripoti toka kwa waziri mwenye dhamana ila ripoti tayari imekabidhiwa kwa Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ataipeleka kwa waziri kwa ajili ya hatua stahiki,” alisema Dk Malima.
Alisema kamati hiyo iliundwa na Mganga Mkuu wa Serikali kwa agizo la Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mwanamke huyo.
Alisema kamati ilifanya uchunguzi kwa muda wa wiki moja imekabidhi ripoti Ijumaa ya wiki iliyopita.
Hata hivyo, juhudi za kumpata Dk Kingwangala hazikufanikiwa baada ya simu yake kutopokelewa kwa siku nzima ya jana.
Asma ambaye alijifungua kwa njia ya upasuaji kwenye Hospitali ya Temeke Machi 17 na kuambiwa alikuwa na mtoto mmoja, alidai vipimo alivyofanyiwa kwenye Zahanati ya Huruma pia madaktari wawili wa Temeke walivithibitisha kwamba ujauzito wake ni wa watoto mapacha.
Alidai licha ya madaktari hao wawili kujiridhisha, lakini baada ya kufanyiwa upasuaji, alipewa mtoto mmoja.
Asma na mumewe Aboubakar Pazi walisema wamewasilisha madai yao kwa uongozi wa hospitali na uchunguzi unafanywa.