MCHAKATO wa Simba kumkabidhi timu mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’, kuwekeza hisa na kufanya mabadiliko kwenye uendeshaji wa klabu hiyo unanukia.
Mo ambaye anataka kuwekeza hisa asilimia 51 zenye thamani ya Sh bilioni 20 na wanachama wa klabu hiyo wamekwishapitisha mabadiliko ya katiba ambapo kwa sasa katiba hiyo ipo kwa msajili ili kubariki mipango hiyo ya Wekundu wa Msimbazi kuendana na mfumo wa uendeshaji soka wa kisasa.
Ingawa mchakato huo ulipingwa na Baraza la Wadhamini wa Simba chini ya Mwenyekiti Hamis Kilomoni, lakini sasa mambo yanaonekana kwenda vizuri baada ya baraza hilo kukaa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, kujadili mchakato huo na kusikiliza hoja za mapendekezo ya klabu hiyo kumilikishwa.
Waziri Mwakyembe alikutana na baraza hilo Aprili 15 mwaka huu mjini Dodoma, likiongozwa na Kilomoni kwa makusudi ya kujadili mchakato wa kubadilisha kutoka klabu ya wanachama na kujiendesha kwa mfumo wa hisa.
Jana waziri huyo alikutana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi na Baraza la Michezo Tanzania (BMT), kujadili mchakato wa umilikishwaji wa klabu ya Simba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Dk. Mwakyembe alisema anaendelea kufanya mazungumzo na viongozi hao kuona klabu hiyo imekwama wapi kutokana na mapendekezo waliyoyatoa.
“Leo jioni (jana) nitakaa na viongozi wa Simba kupata picha kamili ili kuendelea na mchakato huo kama walivyofanya Yanga, ndani ya muda mfupi. Tunataka tufanye mambo mengine haya si masuala ya kutukwamisha, tunahitaji tufanye vizuri zaidi katika masuala haya ya michezo,” alisema.
“Nilishakaa na Baraza la Wadhamini wa Simba kwenye kikao tulichofanya katika ofisi za Uwanja wa Taifa akiwamo Kilomoni na kuwasikiliza nikawaahidi wiki inayokuja nitakaa na viongozi wa klabu yao,” aliongeza Dk. Mwakyembe.
“Kuna mapendekezo ya mabadiliko ya mifumo ya uongozi ya umiliki katika uongozi wetu wa mpira, michakato hiyo imenifikia na mimi nikatamani sana nipate taswira nzima ya suala hili kutoka kwa wenzetu wa BMT, TFF na Msajili wa Vyama vya Michezo.”