SAKATA la pointi tatu za Simba na Kagera Sugar limezidi kuchukua sura mpya, baada ya Wekundu wa Msimbazi, Simba, kubaini mbinu chafu zinazotaka kufanywa na baadhi ya watu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF.
Simba, ambao wamepokwa pointi tatu na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, baada ya kubainika madudu kwenye rufaa yao ya awali iliyojadiliwa na Kamati ya Saa 72, wameendelea kusotea barua ya hukumu yao bila mafanikio kwa siku ya tano sasa.
Akizungumza na BINGWA, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema Simba wameshajua mbinu chafu za TFF, ndiyo maana wao wanasubiri hiyo barua na ndiyo maana hadi sasa TFF wanashindwa kuandika barua hiyo kwa sababu wanataka kupindisha ukweli wa mambo.
“Tunajua kinachoendelea pale TFF, wanataka kufanya mchezo mchafu, mwaka huu hatukubali, tumeomba barua leo ni siku ya tano hakuna chochote mpaka ninavyoongea na wewe hapa, makao makuu ya Simba na TFF hata kwa mguu ni mwendo wa dakika 20 tu, lakini barua haijafika na hukumu na nakala ya maamuzi wanayo,” alisema.
BINGWA lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, Richard Sinamtwa, ili kujua ni wapi barua hiyo imekwama, lakini hakutaka kuzungumza kwa madai kuwa yupo kwenye kikao.
“Nipo kwenye kikao, nipigie baada ya dakika moja,” alisema. Lakini alipopigiwa tena simu yake iliita bila majibu yoyote mpaka tunakwenda mitamboni.
Simba wanataka barua hiyo ili kuweza kupanda ngazi za juu na inadaiwa wanataka kuwasilisha sakata hilo Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Awali Simba ilipewa pointi tatu na Kamati ya Saa 72 baada ya kuwaadhibu Kagera kwa mujibu wa kanuni ya 3 (37) ambayo ilitoa pointi tatu na mabao matatu kwa Simba, ambao kwenye mchezo wa awali walifungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Lakini baadaye Kamati ya Sinamtwa ilitengua maamuzi hayo, baada ya kubainika madudu kwenye rufaa ya Simba, jambo ambalo limewafanya Wekundu hao wa Msimbazi kuwa na matumaini madogo ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Credit - Bingwa
MPIRA UWANJANI NYIE ACHENI HIZO. MNATAKA UBINGWA WA MEZANI!!! ONENI HAYA JAMANI
ReplyDelete