SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ametangaza miezi mitatu ya kile alichoita kuwa ni kuwanyoosha wabunge kitabia huku akitangaza kuingia matatani Freeman Mbowe na Halima Mdee aliowataka wafike mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kuhusiana na tuhuma za kutoa lugha chafu bungeni.
Aidha, Spika Ndugai alisema wameimarisha mitambo ya ulinzi na usalama bungeni ambayo pia wanaitumia kufuatilia mienendo ya wabunge na watu wote wanaoingia kwenye eneo la chombo hicho cha kutunga sheria.
Spika aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akitoa mwongozo kwa wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kangi Lugola (Mwibara) na Joseph Mhagama (Madaba) walioomba mhimili huo uchukue hatua dhidi ya Mbowe, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Spika Ndugai alisema amepokea malalamiko kutoka kwa watu wengi wakimshauri kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Mdee kutokana na Mbunge huyo wa Kawe (Chadema) kudaiwa kutukana bungeni katika kikao cha Jumanne.
"Tumeimarisha sana masuala ya kujua mwenendo wa kila mmoja wetu ndani ya jengo hili na maeneo ya Bunge isipokuwa vyooni. Na yote hii ni kwa sababu ya usalama na ulinzi wenu," Spika Ndugai alisema.
"Niwaambie ninyi mliomzoea Spika… kwa mara nyingine sitachoka kuwaambia tuko hapa kwa miezi mitatu (Aprili 4 hadi Juni 30). Tutashughulika na kila mtu ambaye anajifanya yeye ana vurugu… sasa naanza na Halima Mdee ambaye yeye juzi alimtukana Spika.
"Watanzania wengi wamesikitishwa na jambo hili, wamenipigia, si utaratibu mwema, si utamaduni mwema na hii si mara ya kwanza Halima na hata juzi nilivumilia sana, yaani nilikaa nikasema Mungu anisaidie.
"Baadhi yenu mienendo yetu si mizuri hata kidogo. Kwa hiyo, suala lake nalipeleka mara moja kwenye Kamati ya Maadili iende ikakae. Haiwezekani Bunge hili liwaite watu kwa utovu wa nidhamu halafu lifumbie macho wabunge waliopo humu ndani ambao wana utovu wa nidhamu. Hatuwezi kwenda hivyo.
"Kwa hiyo, Halima Mdee popote alipo katika nchi hii, yeye mwenyewe, najua hayuko Dodoma 'by' saa hizi, kesho muda kama huu (saa 4:23 asubuhi) awe yeye mwenyewe amejileta hapa bungeni la sivyo akamatwe na polisi popote pale alipo ndani ya nchi hii, aletwe kwa pingu hapa bungeni. Hatuwezi kucheza katika mambo ya msingi, tumekuja mmoja mmoja."
Spika pia alimtaka Mbowe kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge kujibu tuhuma zinazomkabili ambazo katika maombi yake kwa mwongozo wa Spika, Lugola alidai kuwa Jumanne iliyopita, kiongozi huyo wa upinzani alitoa lugha chafu dhidi ya Spika na wabunge wa CCM.
"Mbowe pia aripoti kwenye Kamati ya Maadili leo leo, kama yupo Dodoma na baada ya matangazo haya, Kamati ya Maadili iende kukaa immediately (haraka),"alisema Ndugai.
KAULI ZA MBOWE, MDEE
Walipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia uamuzi huo wa Spika, Mbowe na Mdee walisema watatiii agizo lake kwa kufika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Kapteni mstaafu, George Mkuchika.
Baada ya Spika kusitisha shughuli za Bunge jana mchana hadi saa 10 jioni, Mbowe alisema alikuwa kwenye ofisi yake bungeni wakati wabunge wakimshtaki kwa Spika na alisikia kila kitu na atafika mbele ya kamati.
Mbowe alisema: "Sijapata taarifa ya kimaandishi kwamba nakwenda kujibu tuhuma zipi hasa, lakini nitakwenda. Kukutana na kamati hii si mara ya kwanza, kwa hiyo nitakutana na kamati. Siwezi kukataa wito wa kukutana na kamati.
Nitakapokutana na kamati nitajua 'exactly' kosa langu ni nini hasa. Kwa hiyo kwa sasa sitalizungumzia sana jambo hilo maana sina mashtaka rasmi."
Naye Mdee aliiambia Nipashe kwa simu jana akiwa jijini Dar es Salaam kuwa atafika mbele ya kamati hiyo kujibu tuhuma zinazomkabili.
"Nitafika hapo kesho (leo) maana leo (jana) sipo Dodoma. Spika ametoa saa 24, nitazingatia kufika ndani ya muda. Nilikuja Dar es Salaam kwa ajili ya kesi ya uchaguzi wa Meya wa Jiji, kufanya mapokezi ya mwili wa marehemu Macha na kufuatilia hali ya Mheshimiwa Aida aliyegonjwa na pikipiki jana Dodoma na kuhamishiwa Dar kwa ajili ya vipimo zaidi," alisema Mdee.
Credit - Nipashe