Wikienda lilifika kwenye studio hiyo na kuzungumza na chanzo kilichokutwa jirani yake ambapo kilieleza kwamba, tangu alipotekwa Roma na wenzake wakiwa ndani ya studio hiyo huku kompyuta na TV vikichukuliwa na watekaji hao, studio hiyo haijawahi kufunguliwa na haijulikani itafunguliwa lini kwani bado hofu ni kubwa.
“Hofu ni kubwa sana tangu utekaji ufanyike, imebidi studio ifungwe na haijulikani itakuwa wazi lini, ukizingatia waliotekwa bado wako nyumbani wanauguza majeraha waliyoyapata na hali zao bado siyo nzuri hasa Roma,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kupata habari hizo, Wikienda lilimtafuta mmiliki wa studio hiyo anayejulikana kwa jina maarufu la J Murder ambaye alikiri kufungwa kwa studio hiyo na kwamba hajui itafunguliwa lini.
“Tumefunga kwa sababu hatuna vifaa vya kufanyia kazi, kompyuta ndiyo ile iliyoondoka, hatujajua itachukua muda gani ila tukifungua tutawajulisha,” alisema J Murder.
Kwa upande wake Roma anaendelea kuuguza majeraha na bado hajarudi kwenye ubora wake huku polisi wakiendelea na uchunguzi kwenye sakata hilo la utekwaji.