MFANYABIASHARA anayemiliki duka la vipuri vya magari mjini Tarime, Tumaini Wankyo (28) maarufu Zuma, amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) Kikosi cha Nyandoto, Rojar Elias kwa kumpiga risasi wakati wakigombea mwanamke wakiwa hoteli na baa ya NK mjini Tarime mkoani Mara.
Jaji Joaquine De-Mello alitoa hukumu hiyo jana katika kesi namba 9/2016 katika kikao cha Mahakama Kuu inayoendesha vikao vyakeMahakama ya Wilaya Tarime. Awali, Mwanasheria wa Serikali, Harry Mbogoro alidai kuwa Agosti 17, 2015 saa 7 usiku Wankyo akiwa katika Hoteli ya NK iliyopo mjini Tarime akiwa na mpenzi wake wakila chakula na vinywaji, alifika askari wa JWTZ, Elias akiwa na wenzake wawili na kutaka kumchukua mwanamke aliyekuwa naye Jacob.
Alidai alimshambulia kwa kumpiga ngwala na kumwangusha chini, na mtuhumiwa alitaka kujiokoa akiwa ameangushwa chini huku akiwa na silaha yake na risasi iliyokuwa ndani ya bastola yake anayomiliki kihalali, ilifyatuka na kumjeruhi Elias aliyekimbizwa Hospitali ya Wilaya Tarime kisha kuhamishiwa Hospitali ya Bugando jijini Mwanza ambako alifariki wakati akipatiwa matibabu.
“Mtuhumiwa baada ya tukio hilo usiku huo alifika Kituo cha Polisi Tarime akiwa na majeraha aliyopigwa wakati wa ugomvi na askari hao na kupewa PF 3 ya kupatiwa matibabu na kusalimisha silaha yake na baadaye kuwekwa chini ya ulinzi na kushitakiwa kwa kuua bila kukusudia amekaa rumande kwa miezi sita na kupewa dhamana,” alidai mwanasheria huyo wa serikali.
Wakili wa upande wa utetezi, Deus Mgengeri alimtetea mteja wake kuwa mtuhumiwa walikuwa hawana chuki wala fitina yoyote na marehemu, bali ni ugomvi uliotokana na kugonganishwa na mwanamke na kumshambulia Tumaini kwa kumpiga ngwara na kumuangusha chini akiwa na wenzake ambapo mtuhumiwa alitaka kujiokoa na kipigo kutoka kwa askari hao.
Hana rekodi mbaya ya makosa ya jinai na ni kosa lake la kwanza, hivyo akaomba Mahakama kumpa adhabu ndogo mteja wake. Jaji De-Mello alimhukumu mshitakiwa kwenda jela mwaka mmoja ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Chanzo: Habari leo