Mkazi wa Kijiji cha Keisangora, Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Mwita Magige, amekatwa mkono wa kushoto kwa kile kinachodaiwa kushindwa kulipa deni la sh 300,000 baada ya ng’ombe wake wane kukamatwa na mdeni wake.
Tukio hilo lilitokea kijijini hapo baada ya ng’ombe wake waliokuwa wakichungwa na mkewe kukamatwa na mdeni wake ili kumshinikiza amlipe.
Magige alisema, Aprili 5 akiwa safarini alipigiwa simu kuwa mifugo yake imekamatwa na uongozi wa Kijiji na alitakiwa kwenda kuikomboa, baada ya hapo alisitisha safari na kurejea nyumbani, alikwenda kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Nuru Magacha alimweleza kuwa mifugo yake ipo na anadaiwa sh 300,000.
Magige alisema muda mfupi baadaye yowe lilipigwa kuashiria hatari na kwamba, akiwa hajui kinachoendelea wananchi walikusanyika na kijana mmoja alimkata mkono wa kushoto kwa panga na kuucha ukining’inia.