Tumemsikia Roma..ila Maswali Bado ni Mengi


TUMEMSIKIA ROMA

Roma au Rhymes Of Magic Attraction wa Mkatoliki, amezungumza. Ameeleza alichonacho kuhusu tukio lao la kutekwa kisha kupatikana Jumamosi, siku moja kabla ya ile ambayo iliahidiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Dar.

Kinyume na ahadi ya Mwenyekiti kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara na kwamba vingempata kabla ya Jumapili, wale watekaji wenyewe walimwachia Roma na wenzake watatu. Bila shaka hao watekaji watakuwa waliusikia mkwara Mwenyekiti wakaingia mitini.

Bado una maswali hata baada ya kumsikiliza Roma? Nakwambia Roma alitekwa, wewe ukibisha endelea kukomaa na ubishi wako.

Waliomteka ni akina nani? Je, ni majambazi? Basi hao ni majambazi wa aina yake, ambao wanawachukua watu na kukaa nao siku tatu wakiwafanyia mahojiano kisha wanawaachia baada ya kuwatesa. Nasisitiza, hao ni majambazi wa aina yake.

Waliomteka siyo vyombo vya dola, ndiyo vyombo vya dola havihusiki, ila akina Roma walifungwa pingu, walipewa mkong’oto na kuhojiwa. Nasisitiza, vyombo vya dola havihusiki.

Walitekwa na watekaji wa kukodi? Sawa kama ndivyo hivyo, hao watekaji eti hawakupewa hata picha ya wanayemtafuta. Rejea maelezo ya awali ya CEO wa Tongwe Records, J Murder kuwa watekaji walipofika studio walimuulizia yeye pamoja na Roma ambaye alikuwepo ila hawakumtambua. Nasisitiza, hao ni watekaji wa aina yake.

Wewe unaamini Roma na wenzake walijiteka? Kuamini hivyo ni aina nyingine ya uzezeta wa kufikiri. Kama ni rahisi na wewe jipeleke wakupe kisago, wakuvunjevunje, wakutoe majeraha, wakukate jino moja halafu wakupe Dola 5,000 ugawane na wenzako. Nasisitiza, jaribu wewe uone kama ni rahisi.

Wewe unaamini ni mchongo? Unapoamini hivyo unathibitisha ule utafiti wa kila Watanzania wanne mmoja ni kichaa ambaye ni wewe. Mjinga gani mwenye kupanga soo na watu wanne ili wapige pesa? Kuna siri hapo? Halafu wanne wote wa kazi gani? Kwa nini wasimalizane na Roma peke yake? Nasisitiza, wewe ni mmoja katika wale wanne.

Jiuliza, wale watu waliwaulizia Roma na J Murder ambaye hakuwepo. Je, wangewakamata Roma na J Murder peke yao ingekuwaje? Inawezekana wameachiwa kwa sababu mpango ulifeli baada ya Murder kukosekana.

Hali si shwari

By @luqmanmaloto
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad