Uhasama wa Taifa la Marekana na Korea Ulipoanzia


Mpaka nusu ya kwanza ya Karne ya 19 ilipokuwa inaelekea kukamilika, Korea ilikuwa moja. Nchi hiyo iligawanywa mara mbili na Marekani pamoja na Urusi kupitia iliyokuwa dola ya Umoja wa Nchi za Kisovieti (USSR). Kuanzia mwaka 1910 mpaka nyakati za mwisho za kukamilika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Korea ilikuwa imekaliwa na Japan. Baada ya Japan kuwa mahututi kutokana na athari za Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Marekani na Urusi waliamua kuikomboa Korea.

Japan ilikuwa imetoka kupigwa maeneo mengi iliyokuwa imeyashikilia, vilevile ilikuwa inaugulia maumivu ya shambulio la nyuklia, iliyopigwa na Marekani katika miji ya Hiroshima na Nagasaki, kisha athari yake ko mengi wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Hata mpaka wa kuigawa Korea katika pande mbili ni makubaliano ya Urusi na Marekani. Walichora mpaka, wakauita 38th Parallel kisha Urusi ikaipiga Japan upande wa Kaskazini na kuikamata Korea Kaskazini, halafu Marekani ikaiondosha Japan Kusini, hivyo kuishika Korea Kusini.

Kwa ukombozi huo, Urusi iliijaza upepo dola ya Korea Kaskazini kujitangaza kuwa yenyewe ndiyo Serikali ya Korea yote. Marekani nayo, ilishawishi Korea Kusini kupitia mamlaka zake, kujitambulisha kuwa dola ya jumla katika Korea nzima.

Athari za Urusi na Marekani zilionekana kupitia mifumo yake ya kiuchumi. Urusi kwa sababu ni Wajamaa, waliiambukiza Korea Kaskazini mfumo wa Ujamaa. Marekani na Ubepari wao, waliigeuza Korea Kusini kuwa nchi ya kibepari.

Hivyo basi, Korea Kaskazini tangu kuasisiwa kwake na kutambulika rasmi kama dola ya Jamhuri ya Watu wa Kidemokrasia wa Korea (DPRK), haiivi na Marekani. Viongozi wake wamekuwa jeuri kweli dhidi ya Marekani.

Siku zote, imani ya Marekani ni kuwa Korea Kaskazini inakumbatiwa na Urusi pamoja na China, mataifa ambayo ni mahasimu wake katika safari ya tamaa ya kuitawala dunia kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia na kijeshi.

Ni kama ambavyo Korea Kaskazini, China na Urusi, huamini kuwa Marekani inaipa Korea Kusini nguvu za kiuchumi na kiteknolojia ili istawi zaidi ya Korea Kaskazini, kisha huo uwe mfano dhahiri wa kushindwa kwa China na Urusi.

Tuendelee na mgogoro wa silaha za nyuklia kati ya Marekani na Korea Kaskazini.

Nakumbusha pia kuwa Marekani ndiyo huibeba Korea Kusini. Nilieleza kuwa Urusi na Marekani ndiyo sababu ya Korea kugawanywa Kusini na Kaskazini
ENDELEA SASA
Chokochoko za Marekani, Urusi na China ni sababu ya Vita ya Korea kuanzia mwaka 1950 mpaka 1953. Korea Kusini ilishawishiwa kujitangaza kuwa Serikali ya Korea nzima, vilevile Korea Kaskazini ilitakiwa kujitangaza kuwa mtawala wa dola nzima ya Korea.

Mwanzo wa Vita ya Korea ni Marekani kuitangaza Korea Kaskazini kuwa iliivamia Korea Kusini, hivyo mapambano yalianza. Awali ilionekana kama Marekani isingetumia msuli mkubwa kuikabili Korea Kaskazini.

Hata hivyo, Marekani ikiwa imeweka kambi ya vita ambayo hufahamika kama Chosin Reservoir Campaign, Novemba 27, 1950, ilishambuliwa kwa kushtukizwa na China, hivyo mapigano makali yalitokea.

China iliamua kuishambulia Marekani ili kuudhoofisha mpango wake wa kuipiga Korea Kaskazini. Mapambano hayo ambayo yalidumu kwa siku 16 kati ya China na Marekani, huitwa Battle of Chosin Reservoir. Yalianza Novemba 27 mpaka Desemba 13, 1950.

Battle of Chosin Reservoir shabaha kuu ilikuwa ni China kuimaliza nguvu Marekani mapema, lakini baadaye vikosi vya Umoja wa Mataifa, Uingereza na Korea Kusini, waliungana na Marekani kuikabili China.

Kuanzia hapo moto ukawaka jumla katika Vita ya Korea, kufikia wakati huo ikawa ni Korea Kaskazini dhidi ya Korea Kusini. Vikosi vya Umoja wa Mataifa, Marekani, Uingereza, Canada na mataifa mengine washirika walikuwa upande wa Korea Kusini.

Upande wa Korea Kaskazini kulikuwa na China, Urusi (USSR), Ujerumani Mashariki, Bulgaria, Jamhuri ya Czech na mataifa mengine ambayo ni washirika wa mfumo wa kiuchumi wa kijamaa.

Mwisho kabisa, utaona kuwa tafsiri ya Vita ya Korea ni uhasimu wa kihistoria kati ya Ujamaa dhidi ya Ubepari. Korea Kaskazini na Korea Kusini ni nchi ndogo lakini ziligonganisha wababe wa dunia kwa sababu za kimaslahi kati ya Ujamaa na Ubepari.

Ndimi Luqman MALOTO
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad