ATHUMANI Omary ambaye Sasa ni gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti kama Harmorapa, ni msanii ambaye amekuja na bahati ambayo wengi wameshindwa kuipata, hata baada ya miaka kadhaa ya kuhangaikia jina kwenye Muziki wa Kizazi Kipya.
Wapo wanaoamini katika bahati na wengine wanajaribu kumhusisha meneja wake, Irene kuwa ndiye aliye nyuma ya matukio yote yanayoendelea kumhusisha msanii huyo ambaye ana nyimbo mbili tu kwenye gemu, Kiboko ya Mabishoo ukiwa ndiyo wenye kupigwa zaidi, kutokana na kumshirikisha mkongwe Juma Kassim ‘Nature’. Kijana huyu mdogo kiumri, anaonyesha wazi kuwa amekuja mjini kutafuta, kwani hana aibu na wala hajisikii vibaya.
Yupo tayari wakati wowote kusimama mbele ya kamera na kujibu chochote anachoulizwa, ingawa ukimsikiliza kwa makini, unagundua kuwa siyo mjuzi wa mambo mengi anayoyazungumzia.
Tofauti na wasanii wenzake ambao walianza kujulikana kidogokidogo kutokana na kazi zao kupata mashiko masikioni mwa mashabiki, kijana huyu kutoka Kusini mwa nchi yetu ameibuka tu ghafla akiwa hana kazi yoyote ‘mezani’.
Kilichomuibua, ni kule kufanana kusiko kawaida na chipukizi mwenzake, Abdulhan Rajab ‘Harmonize’. Na ndiyo maana nikasema pale mwanzo kuwa kijana huyu ana bahati, kwa sababu kama kufanana na mtu ni tiketi ya kupata jina na umaarufu, wamewahi kutokea watu kibao waliofananishwa na mastaa.
Kuna jamaa alifanana ‘mbaya’ na Ngwair, lakini hajawahi kupata kiki kupitia ufanano huo. Wapo pia waliowahi kufananishwa na akina Ray C, Wema Sepetu na wengineo kibao. Na utakubaliana na mimi kuwa hii ni bahati ya mtende kwa Harmorapa, mwangalie Harmonize mwenyewe, siyo msanii mkubwa kivile, ni dogo tu mmoja hivi aliyepata jina kwa sababu ya Diamond, ingawa anajitahidi kufanya kazi.
Kinachonisikitisha, ni hii tabia ambayo inaonekana wale walio nyuma ya Harmorapa wanadhani itamsaidia kumfanya aendelee kuwa ‘talk of the town’. Amekuwa mtu wa matukio na maigizo zaidi, badala ya kufanya kazi anayoipenda.
Angekuwa makini, hiki kilikuwa ni kipindi kizuri kwake, cha kukaa muda mwingi studio na kufanya kazi nzuri, kwa sababu tayari ana watu wanasubiri kusikia anaimba nini. Lakini yeye amebakia kuwa mtu wa vichekesho, anayeendeshwa na matukio.
Leo ataonekana huku akifanya hivi, kesho yake yupo kule akiwa na flani, ili mradi tu watu wacheke. Angalia, mara tu baada ya kusikika kwa taarifa ya kifo cha kiongozi wa Freemasons Bongo, Andy Chande, watu wanadai kijana huyo mwenyeji wa Masasi alikuwa njiani kwenda kuwafariji wafi wa! Hii maana yake ni kebehi, watu hawamuoni kama mwanamuziki, bali mtu wa vituko.
Na siamini kama ana washauri, maana kama ushauri wenyewe ndiyo ule wa kumfanya ageuke kituko, basi hawajui. Wangemshauri awe comedian, aachane na muziki. Na muda unakimbia, kama ana watu nyuma yake wana matumaini ya kuja ‘kula kuku’ kupitia muziki wake, wamshauri achague moja, muziki au vichekesho.
Na akichagua, afanye hima kabla wakati haujamuacha, maana kwa staili ya maisha aliyoichagua, baada ya kejeli anazochukua hivi sasa, mashabiki wataanza kumdharau na huo ndiyo utakuwa mwisho wake.
Harmorapa anaweza kuwa msanii wa vichekesho na mkono ukaenda kinywani kama wanavyofanya wenzake akina Steve Nyerere, MC Pilipili, Idris Sultan, King Majuto na wengine wa aina hiyo, kwa sababu jina ameshapata na kipaji cha kuvunja watu mbavu kwa vituko anacho, lakini kama ni muziki, kwa staili hii, asahau kutoboa!