Kuna kitu ambacho Rais amekuwa akikisema mara kwa mara na ninaamini kuna ukweli wake. Kwamba, siyo wote wanaolalamikia utawala wake wanafanya hivyo kwa sababu wanataka afanikiwe. Ni kweli pia kuwa wapo wanaolalamika kwa sababu wanafikiri kuna labda namna bora ya kufanya mambo fulani fulani. Lakini, kuna masuala ambayo anayafanya ambayo bila ya shaka Watanzania wako nyuma yake.
"Tulionewa sana
Tumechezewa sana
Tumedharauliwa mno"
Siku ya Krismasi ya mwaka juzi gari langu dogo la Nissan Maxima lilizimika kwenye eneo la kuegeshea magari hapo hapo kanisani. Bahati nzuri nyumba yangu ni dakika kumi tu kutembea kutoka kanisani. Kila namna ya kuliwasha tena haikuwezekana. Nilipowaita mafundi wakaniambia tu kuwa injini imekufa! Hakukuwa na jinsi isipokuwa kuweka injini nyingine!
Kuna ukweli kwamba wakati mwingine hata gari zuri kiasi gani inabidi ulipeleke kufanyiwa matengenezo ya kawaida. Lakini, kuna wakati gari linahitaji matengenezo makubwa. Katika kufanya matengezo makubwa gari linaweza kukongolewa kabisa, injini kushushwa, vilivyochakaa kutolewa, n.k Mtu yeyote atakayeliona gari likiwa kwenye matengenezo makubwa anaweza kudhania ndio mwisho wake; kwamba limeharibiwa. Lakini likiunganishwa tena na kuanza kazi linakuwa katika ubora zaidi kuliko wa awali. Sasa watu wakilalamika tu kusema kuwa gari limeharibiwa wanaweza kuwa sahihi kwa sababu wanaweka mkazo katika mwonekano likiwa kwenye matengenezo!
Kazi kubwa kwa Magufuli ni kuwafanya watu waamini kuwa analitengeneza gari hilo na kuwa matengenezo haya ni kwa ajili ya ubora wa baadaye. Na kwamba katika kufanya hili hatoonea huruma kuondoa visivyo faa na hata ikibidi kuishusha injini na kuweka injini nyingine. Katika matengenezo ambayo anaendelea kuyafanya Tanzania ambayo sisi wengine tuliyaita "mabadiliko ya kweli" na sasa naomba kupendekeza yaitwe pia "mabadiliko sahihi"kuna vitu ambayo anatakiwa kuendelea navyo na kuvifanya vizuri zaidi lakini kuna vingine ni lazima avifanye kama hivyo vingine vinatakiwa kufanikiwa.
Kufumua Idara ya Usalama wa Taifa ni moja ya mambo muhimu sana ya kuweza kufanikisha maeneo mengine yote. Mgonjwa wa moyo hata kama ana matatizo mengine ya mguu na meno; au hata kama ana matatizo ya tumbo; anaweza kuyashughulikia hayo mengine yote lakini bila kushughulikia tatizo kubwa la moyo mengine yanaweza kushughulikiwa lakini mwisho wa siku ni moyo utakaoamua kama hayo mengine yana nafasi ya kufanikiwa! Usalama wa Taifa ni moyo wa taifa! Hautakiwi hata kwa siku moja uonekane unapiga kwa matatizo, au una matatizo mengine...
Inshallah, wiki ijayo nitaendeleza hoja hii ya mabadiliko makubwa ya Idara. Tusisubiri watu wa nje watushunikishe kufanya mabadiliko. Baba wa Taifa alikuwa na msemo ambao wengi labda wameusahau (hii ilikuwa mara baada ya uhuru) kuwa "Tanzania ni ya Watanzania na Watanzania ni Wote - Tanzania is for Tanzanians and Tanzanians are All". Msemo huu ulikuwa unasisitiza tu kuwa hakuna mwenye Utanzania zaidi ya Watanzania wengine. Kila Mtanzania - haijalishi kabila, dini, rangi, uwezo, hadhi, mahali, hali au umbali - ana haki sawa na Mtanzania mwingine yeyote. Hakuna Mtanzania wa juu zaidi!