MUZIKI ni sanaa pana inayohitaji zaidi akili iliyotulia ili kuifanya kuwa bora na isiyokufa. Ni wanamuziki wachache wamewahi kumudu kuifanya kazi yao kuwa ya muda wote kwa nyakati zote, bila kujali vizazi vinavyokuja na kupotea, vinavyochagizwa na kukua kwa teknolojia.
Katika kundi la wanamuziki wa aina hiyo, unamkuta Robert Nesta Marley, ambaye wengi tumezoea kumwita Bob Marley. Ingawa alifariki mwaka 1981, ndiye mwanamuziki wa Reggae anayefahamika kuliko wengine wote, wakiwemo wanaoimba hivi sasa!
Wakati Marijani Rajab ‘Jabali la Muziki’ akiimba kibao cha Geogina miaka mingi iliyopita, hakujua kama leo hii, vijana waliozaliwa miaka ya themanini na tisini wanacheza na kuimba kibao chake kana kwamba kimeimbwa na akina Khalid Chokoraa! Hata hivyo, sanaa ya muziki pia inatambua umahiri wa watu wanaoimba kwa masilahi ya nyakati za kizazi chao, iwe kwa ajili ya kuiburudisha jamii inayomzunguka, kufundisha, kuhadharisha na madhumuni mengine kedekede.
Katika kundi hili, kwa wanamuziki wetu wa kizazi kipya, tunao wengi wanaostahili tuzo. Wanafanya muziki wao kwa faida ya kizazi chao cha sasa, mashabiki wanapata burudani, wanapewa hadhari, wanafundishwa na wakati mwingine hata kushauriwa.
Hivi karibuni, Hamis Mwinjuma maarufu kama FA, alisema Rais Magufuli alimpigia simu na kumweleza kuwa yeye ni shabiki wa muziki wake na kuwa anakifagilia sana kibao chake kilichopo mtaani kwa sasa, Mwanaume Suruali! MwanaFA ni mmoja wa marapa wazuri, lakini yeye siyo mkosoaji wa watawala na wala hajishughulishi na nyimbo zenye mlengo wa siasa, ingawa ana uelewa wa hali ya juu katika mambo ya siasa kuliko wasanii wengi.
Kama Rais ameruhusu Wimbo wa Wapo upigwe redioni na tena anaupenda wimbo wa MwanaFa wa Mwanaume Suruali, Roma amefanya nini? Waliomteka hawawezi kuwa mawakala wa serikali kwa sababu hatuoni katika wimbo upi watawala wamekwazika.
Waliomteka hawakuwa na nia ya kumuua, ila kuna kitu tusichokijua walihitaji kukifahamu kutoka kwake. Kama nilivyosema mwanzo, Roma ni jasiri. Anajua kama watu hawakutosheka na alichokisema kwenye ile press conference kwa sababu yule siyo Roma wanayemjua.
Mashabiki wanasubiri Roma awaeleze ukweli kwa sababu hawaamini kama ile ni sinema ya kutafuta kiki.
Hata yeye mwenyewe anajua kama hakuwashibisha. Na bahati mbaya ni kwamba wote wanajua siku ile hakusema walichotaka kukisikia na kinachosikitisha zaidi ni kuwa hata akirejea tena na kuongopa, watajua wamedanganywa.