Hali si nzuri katika sekta mbalimbali baada ya baadhi ya biashara kufungwa, kampuni kupunguza wafanyakazi na bidhaa kupanda bei, imeelezwa.
Hali hiyo inaashiria kudorora kwa uchumi huku baadhi wakiihusisha na uwapo wa sera zisizo rafiki kwa ukuaji wa uchumi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye baadhi ya masoko hapa nchini umebaini kuwa bidhaa mbalimbali zimepanda bei yakiwamo maharage ambayo yamepanda kutoka Sh1, 800 hadi kati ya Sh2, 700 na 3,000 kwa kilo.
Pia, sukari imepanda kutoka bei elekezi iliyotolewa na Serikali ya Sh1, 800 hadi Sh2,500, mchele kutoka Sh1,200 hadi 2,600 kwa kilo.
Unga wa sembe nao umepanda kutoka Sh1, 200 hadi Sh 2,000. Bidhaa nyingine zilizopanda ni mboga za majani ambapo fungu la mchicha, chainizi, tembele limepanda kutoka Sh200 hadi Sh400 na Sh500.
Hali hiyo inasadifiwa na ripoti za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinazobainisha kuwa kasi ya mfumuko wa bei imekuwa ikiongezeka mwezi hadi mwezi kutoka asilimia 4.8 Novemba mwaka jana hadi asilimia 6.4 kwa mwaka unaoishia Machi mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Francis Nanai amesema kampuni hiyo imepunguza wafanyakazi kwa asilimia nane na kusimamisha ajira zote zilizokuwa zimeidhinishwa mwaka 2016/2017.
TDL ambayo ni kampuni tanzu ya Tanzania Breweries Limited (TBL) nayo mapema Machi 27 mwaka huu ilitangaza kupunguza wafanyakazi wake wasiozidi 50 ili kukabiliana na hali ya kiuchumi.