WAKATI biashara zikikwama, benki zikiyumba, baadhi ya viwanda kufungwa na vingine kupunguza wafanyakazi huku wananchi waliokopa ili kupata fedha kusaidia kuendesha maisha wakishindwa kufanya marejesho, wasomi nchini wamesema mambo hayo yanatokana na mfumo ‘mbovu’ wa ulipaji kodi na kuyumba kwa sekta binafsi.
Kwa hali hiyo, wameshauri wananchi walioachishwa kazi kutumia elimu yao kujiajiri, kujitosa katika kilimo na kuitaka Serikali kushirikisha sekta binafsi katika shughuli zake na kuachana na utaratibu wa kukumbatia kila kitu, kwa maelezo kuwa unasababisha fedha kutokuwa kwenye mzunguko.
“Mtu anaweza kubambikiwa kodi… unajua Sheria ya Kodi inataka mtu akitajiwa kiasi cha kulipa alipe tu hata kama si cha kweli. Ni lazima alipe robo tatu ya kodi hiyo, ndipo akate rufaa jambo ambalo watu wengi wanashindwa,” alisema Dk Christopher Awinia, Mkurugenzi wa Kituo cha Uchumi na Maendeleo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani amekuwa akihimiza kila mtu kufanya kazi ili kujipatia kipato ambacho kitamwezesha kulipa kodi halali.
Hali hiyo iliambatana na kupambana na ufisadi, kufuatilia wakwepa kodi, kufuta posho na mikutano ya Serikali hotelini, kudhibiti safari za ndani na nje ya nchi zisizo na umuhimu sambamba na fedha zote za mashirika ama taasisi zake kuhifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mikakati hiyo inayodaiwa na baadhi ya wananchi kuwa ndio imesababisha ugumu wa maisha, ndio iliyotolewa mfano na wachumi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti.
Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) alisema: “Kwa sasa tunachokiona ni Serikali kuonekana kutotaka fedha zake ziende kwenye mikono ya sekta binafsi. Tatizo limeanzia hapo.
“Haitaki fedha ziende benki na kampuni binafsi. Mfano Serikali inahamia Dodoma na kuhamisha vitu vyake, lakini inatumia majeshi badala ya watu binafsi ambao watalipwa fedha zitakazoingia kwenye mfumo.”
Alisema anachokiona sasa ni sekta binafsi ambayo ndiyo inaajiri idadi kubwa ya wananchi, kukabwa shingo, “haya matatizo yanayotokea yalitarajiwa. Hatuwezi kuyashangaa kama Serikali haitaruhusu fedha zake kuingia kwenye mfumo.”
Alisema suluhisho ni Serikali kutumia sekta binafsi na kulipa madeni wanayodaiwa na makandarasi ili fedha ziingie kwenye mzunguko.
Alibainisha kuwa wapo wanaodhani kuwa hali inayotokea sasa ni kubadilika kwa utaratibu wa kuendesha uchumi kutokana na watu kuishi kwa kutegemea ‘dili’ ambazo kwa sasa zimeyeyuka.
“Wapo pia wanaodhani kuwa yanayotokea sasa ni mambo ya mpito tu. Wapo wanaodhani uendeshaji wa uchumi kwa sasa ndio uliozalisha matatizo haya,” alisema.
Profesa Gabagambi alisisitiza kuwa katika mfumo ambao Serikali inabana matumizi, inapata faida kwa kukusanya kodi zaidi na kupunguza mfumuko wa bei, lakini kinadharia kuna uhusiano wa wa karibu kati ya kupunguza mfumuko wa bei na kuongeza tatizo la ajira.
“Ni matatizo mawili ambayo ni pacha, lakini yanakwenda kinyume. Ukiongeza ajira huibuka mfumuko wa bei na ukidhibiti mfumuko wa bei lazima litaibuka tatizo la ajira,” alisema msomi huyo.
Alisema umefikia wakati wenye elimu kuitumia kujiajiri sambamba na wengine kujitosa kwenye kilimo, kuliko kusubiri ajira kutoka serikalini na sekta binafsi.
Dk Awinia aliungana na Profesa Gabagambi na kusisitiza kuwa katika ulipaji kodi wa aina hiyo, wengi husimamisha biashara zao jambo ambalo linasababisha watu kupunguzwa kazi.
Akitolea mfano kusitishwa kwa viwanda kuzalisha vinywaji na kuweka kwenye mifuko ya plastiki maarufu kama viroba, alisema: “Watashindwa kuajiri watu kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. Serikali inapaswa kuangalia sera iliyopo kama ina tija.”
Alisema ili kunusuru hali hiyo, Serikali inapaswa kuwa na mjadala na wadau wa sekta binafsi ili kujua njia ya kutatua changamoto ili mazingira ya kuwekeza na biashara kuwa mazuri kwa kuzingatia mwelekeo wa Bajeti.
Akizungumzia kodi, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Godbether Kinyondo alisema suala la kulipa kodi halikwepeki na kushauri wananchi kuelekeza nguvu zao kwenye ujasiriamali ili kuweza kumudu hali ngumu ya maisha.
“Hakuna shaka kuwa usimamizi katika kodi ndio sababu lakini hakuna jinsi kama ulikuwa unadanganya katika ulipaji kodi sasa utailipa na unaweza kushindwa kuendeleza kampuni yako,” alisema.
Alisema asilimia kubwa ya wafanyabiashara hawapo tayari kupata hasara, hivyo baada ya kubanwa katika kodi wanachukua uamuzi wa kupunguza wafanyakazi ili wapate faida.
Tukiendelea kuzuia Dili za hawa wajanja wajanja..tumeua mchezo
ReplyDelete