Kwa siku nne zilizopita kumekuwa na taharuki baada ya ‘kutekwa’ kwa wasanii wa Bongo Fleva, Roma, Moni na wenzie lakini habari njema ni kuwa kwa sasa wamepatikana. Tukio hilo limezua mijadala mingi katika mitandao ya kijamii.
Wakati mijadala ikiwa inaendea na watu kuhoji wapi alipo Roma na wenzie, msanii anayesifika na kuheshimika nchini, Diamond Platnumz anatoa wimbo ‘Acha Nikae Kimya.’
Wimbo huo umekuja kukoleza mijadala iliyokuwa inaendelea, watu wanauhusisha tukio la kupotea wakina Roma. Binafsi nimesikiliza wimbo huo nikubaini kwa nini umezoa mjadala.
Mosi: Diamond ameshindwa kuficha hisia zake dhidi ya RC ambaye ni kipenzi chake, kuna mstari anasema ‘Napewa za chini ya kapeti kuna redio imevamiwa eti Ehh, napita kwenye magazeti nakuta lundo la watu wameketi Ehh, badala ya kutafuta senti wanabishana tu mambo ya vyeti’.
Kabla ya kuandika makala haya, kupitia account yangu ya twitter niliandika ‘Diamond asicheze na akili zetu….,’. Hata sasa naweza kurudia hivyo, Diamond asicheze na akili zetu.
Kwa tafsiri pana ya hiyo mistari hapo juu, ni kwamba yeye hajui kuhusu tuhuma za RC kuvamia kituo cha redio/TV pia ndani yake kuna kubeza tuhuma hizo, be intellectual.
Pia nimesikia amegusia kuhusu vyeti na kuwashangaa wanaohoji suala hilo badala yake watafute fedha, well in god. Nimpongeze kwa hilo maana hata mimi sipendi watu wanaokaa vijiweni/vibanda vya magazeti na kuongea udaku tu bila kufanya kazi.
Lakini tuhuma za kughushi vyeti tena kwa kiongozi ambaye anaongoza kundi kubwa la watu katika jamii ni wajibu wa wale anaowangoza kuhoji, wala hakuna ubaya, udaku au kupoteza muda wa kutafuta senti kama wewe unavyodai. Hapa mchezo ni simple tu kama kumsukuma mlevi, anayetuhimiwa ajitokeze akanushe na maisha yaendelee.
Jambo la pili linaloleta mjadala kuhusu wimbo huu ni suala la Roma, ‘ahh, ohh Tanzania Mara kimbembe Dodoma wabunge pinzani wamegoma juzi akapotea na Roma,’, ni moja lines. Nimejiuliza maswali mengi sana, kwanini huu wimbo utoke muda huu na si wiki iliyopita au mwezi ujao, Diamond asije akatudanganya alikuwa ameurekodi siku nyingi maana Roma na mwenzie ‘wametoweka’ wiki hii, ina maana wimbo umeandikwa na kurekodiwa wiki hii. Jaribu kuwaza kwa sauti, narudia tena, jaribu kuwaza kwa sauti.
Siukatai wimbo wake, kwani ameimba vizuri, melody nzuri, beat nzuri, ujumbe unahasisha uzalendo na kuwa na busara lakini kuna mambo ambayo yananipa ukakasi. Ila pongezi kwake
MAWAZO YANGU
Yeye kama msanii ambaye ni kioo cha jamii anatakiwa kusema shida za wengi, yaani kuwakilisha kundi kubwa la watu. Kujali maslahi binafsi ni kujiharibia.