JAMANI wasomaji wangu, mimi kila wiki ikifika Alhamisi msemo wangu ni uleule kwamba, Mungu ni wa kumshukuru sana kwa sababu kila ninapopitia makosa yangu kwa wiki, halafu bado ameniacha kuishi, naumia sana.
Naumia zaidi ninaposikia mtu wangu wa karibu ambaye namfahamu hata kwa matendo yake kwamba, alikuwa mtu mwema kuliko mimi, lakini yeye ametangulia mimi mwovu nimebaki, namuogopa sana Mungu.
Mungu bwana hana ajabu yoyote kama wengi wanavyosema eti Mungu ni wa ajabu, si kweli. Bali yeye Mungu ndiye ajabu! Yaani si Mungu wa ajabu bali Mungu ndiye ajabu! Alhamisi ya leo nataka kuzungumzia ishu ya waheshimiwa wabunge.
Kwanza nawapongeza sana kwa sababu, kusema ule ukweli wabunge wa mwaka huu si kama wa miaka ya zamani. Wabunge wa sasa wanajua kazi yao, wanakwenda bungeni kutetea wanyonge.
Unajua miaka ya zamani, mtu alikuwa anaweza kupata ubunge akiwa na miaka 35, akaendelea kuwa mbunge mpaka ana miaka 75, bado anachaguliwa tu na maendeleo jimboni hapeleki.
Siku hizi miaka ya wabunge ni mitano tu, usipopeleka maendeleo wanakuangusha, wanamchagua mwingine. Sasa mimi nilichojifunza ni kwamba, katika wabunge mia moja, sitini na tano wameupata ubunge kwa sababu ya uwezo wa kuongea sana. Jamani!
Nasema hivi kwa sababu moja, nayo ni kwamba, unaweza kukuta mbunge amepewa nafasi na mheshimiwa spika ya kuzungumza, basi jamaa anasimama kwenye kipaza sauti na kuanza kusema: “Mheshimiwa spika, kwanza napenda kusema kwamba sitazungumza sana kuhusu kuchangia hilo la makontena ya mchanga wa dhahabu.
Leo nitasema machache tu kwa sababu siko vizuri sana kiafya… “Kwanza kabisa mheshimiwa spika napenda kukupongeza kwa namna unavyoongoza bunge letu tukufu. Wewe umekuwa mfano wa kuigwa kwa kweli. Narudia tena hongera sana…
“Lakini mheshimiwa spika la pili, napenda kumpongeza sana mke wangu, mama Shukuru, yeye kwa kuniwezesha kiafya na matunzo mengine mpaka mimi leo niko hapa mjengoni. Mama Shukuru popote ulipo pokea pongezi zangu…
La tatu mheshimiwa spika napenda kuwapongeza wananchi au wapiga kura wangu wa jimbo langu la Pori Tengefu, kwa kweli nawashukuru sana kwa sababu waliniamini na kunipa ridhaa na leo hii mimi nipo hapa bungeni kwa sababu yao…
“Mheshimiwa spika nne, nigusie kidogo kuhusu hali ya mifugo jimboni kwangu kabla sijaja kwenye hoja ya mchanga wenye dhahabu kwenye makontena uliopigwa marufuku kusafirishwa kwenda nje ya nchi na mheshimiwa mtukufu rais wetu aliyechaguliwa kwa kura nyingi na Watanzania na kuwashinda wapinzani wake ambao sasa wapo wakisubiri uchaguzi ujao wa 2020 kama Mungu atatuweka…”
Spika: “Mheshimiwa muda umekwisha, umebakiza dakika moja tu.” Sasa mimi najiuliza jamani, kama huyu mheshimiwa alisema leo hatasema sana ndiyo kasema hivi mpaka yale aliyotakiwa aongee hakuyaongea, je siku akiamua kusema sana itakuaje?! Mtu anaongea, anatumia madakika kibao kwa shukurani tu wakati hoja ya msingi iko mbele yake, kabla hajaanza kusema dakika zimekwisha. Aaah! Jamani! Anyway, na mimi leo sitasema sana, ngoja niishie hapa!
Time management awareness is the main issue...Tanzania tunahitaji mwamko na hawa mabomu wamechanganyika changanyika Tu. Ni lazima wajiwlewa na wanan hi waelimishwe umuhimu WA kura yake moja inamuathiri vipi mjujui wake huko miaka25 ijayo
ReplyDeleteWell said!bado wananchi wengi wanachagua kwa ushabiki tu na sio kwa tathmini ya ubora wa mgombea.
Delete