Nilikuwa napata elimu kidogo ya kibiashara sehemu, na jambo kubwa lilikuwa namna ambayo Diamond kaja nayo juu ya Perfume yake, nimemfikiria Diamond kwa sababu ni staa kama wanavyoweza kuwa mastaa wa michezo pia wakaanzisha biashara zao.
Swali kubwa lilikuwa bei lakini pia Chapa (brand) aliyoingia nayo sokoni.
1. Bei ya Perfume ya Diamond ni 105000, yaani laki moja na elfu tano. Hii ina maana kuwa wenye uwezo wa kununua hii ni kwa kiasi kikubwa nusu ya wale walioweza kulipa Elfu Hamsini kuingia kwenye show yake Mlimani City. Nasema hivi kwa sababu kwa bei hii kuna brand kubwa Ulaya zenye bei jirani na hiyo ambazo watu wataendelea kuzinunua.
2. Washabiki Wengi wa Diamond ni watanzania. Kipato cha siku cha Mtanzania wa kawaida ninaambiwa hakizidi elfu 70 kwa siku kama tukiamua kukadiria juu sana, lakini wengi wanaishi chini ya Dola 5, yaani elfu 12 hivi. Hii ni changamoto.
3. Biashara ya msanii au staa yoyote ni nadra kuhusishanishwa na kazi yake. Kwa mfano Rihanna viatu vya Fenty vipo chinii ya kampuni kubwa za Puma, sio kwamba hawezi kuanzisha kampuni yake. Air Jordan zipo chini ya Nike, sio kwa sababu hakuweza kuanzisha kampuni, Ronaldo na Pestana Hotels aliingia ubia na wafanyabiashara wakubwa. Msingi wa hili ni kuondoa fikra za watu wanaonuua kuendana na mziki au kipaji chako, ili siku ukishuka ubaki katika soko.
Mikataba ya ushirikiano hii uweka mlinganyo wa kudumu zaidi. Hapa Diamond angeweza kuja chini ya nembo ya kampuni yoyote kubwa, na Fragrance zake zikaitwa hata Armani Chibu, na hii ingefanya Giorigio Arman wafungue kampuni yake nchini.
4. Lakini pia huwa namkubali Diamond kwenye promotion. Sidhani katika hii chibu kama alifanya maandalizi sahihi. Ile amusement na excitement (kufurahia na kuitamani) bidhaa hajaiweka kipindi hiki. Hata yeye mwenyewe hajaonekana katika promo hata kujaribu kuonyesha ina harufu gani, inafaa chumbani kwa namna gani, mtu atafeel vipi akiwa nayo ofisini na mambo mengine ambayo yangevuta wateja wake.
5. Mwisho, bado naamini Diamond ni mpiganaji, kijana wa kipekee na ambaye anajaribu kuleta utofauti wa kufikiri katika kila jambo na kuweka misingi ya fikra za ujasiriamali. Lakini nahisi hili hapa lilichangiwa kwa kiasi kikubwa kuamini katika jina lake kabla ya kufanya utafiti wa walaji wake. Hii ingeambatana na Deodorant na Spray ambazo zingekuwa bei rahisi, angewachota wa Masaki na kwa bibi yangu Magu pale Mwanza.
Mwisho wa siku, bado anahitaji kupongezwa, ni uthubutu wa kipekee huu. Akili yake nimeshindwa kuifananisha na staa yoyote wa Tanzania kwa sasa, katika sekta zote. Hawapo jirani yake, lakini alipoelekea sasa, Menejimenti yake inatakiwa kuwa makini. Uwekezaji huu sio wa muziki sasa, misingi ya uchumi, biashara izingatiwe. Sio kipaji tu huku, ni mahesabu kwelikweli.
Ni mimi mpendasoka Nicasius Agwanda (Coutinho). Nimeandika baada ya kupewa elimu pia.