KIKAO cha kwanza cha Bunge la 11 jana kilisimama kwa dakika 10 baada ya wabunge bila kujali itikadi zao za kisiasa kusimama huku wakipiga meza zao kumshangilia Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye alikwenda bungeni kushuhudia mkewe, Mama Salma akila kiapo cha ubunge.
“Tumekukumbuka, ingia ndani utusalimie, njoo huku ndani utusalimie.” Ni baadhi ya kauli zilizotolewa na wabunge hao baada ya Spika Job Ndugai kumtambulisha Rais mstaafu aliyekuwa ameketi kwenye ukumbi wa wageni wa Spika, muda mfupi baada ya Salma Kikwete kula kiapo.
Wakati wabunge hao wakimshangilia, Rais Kikwete aliyeambatana na mmoja wa watoto wake, Ally, alikuwa akitabasamu na kuwapungia mkono wawakilishi hao wa wananchi, ambao baadhi yao waliwasha vipaza sauti na kutoa hisia zao kwa Rais huyo wa Awamu ya Nne aliyemaliza muhula wa pili wa utawala wake Novemba 2015.
Wabunge
Wabunge waliozungumza na gazeti hili baada ya kikao hicho kuahirishwa, walitaja sababu za kumshangilia Kikwete ikiwamo wakati wa utawala wake uchumi kuwa mzuri, kutokuwepo kwa demokrasia katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano na kuminywa kwa uhuru katika masuala mbalimbali.
“Haijawahi kutokea tangu niwe Mbunge. Hiki ni kipindi changu cha nne kwa mgeni kushangiliwa namna hii,” alisema Ndugai wakati shangwe za wabunge hao zikiendelea.
Wakati shangwe hizo zikiendelea, Ndugai aliwataka wabunge kusimama na kumshangilia Rais huyo mstaafu kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni kumpa heshima kubwa, ombi ambalo lilitekelezwa bila vikwazo na wabunge hao, hata mawaziri.
‘’Kwa makofi hayo sasa naomba mumpe heshima mpigieni makofi mkiwa mmesimama,’’ alisema Ndugai ambaye alichombeza: “Inawezekana waliommiss (waliomkumbuka) nao wapo,” kuonekana kurejea tungo za wimbo uliozua utata unaoitwa ‘Wapo’ ulioimbwa na msanii Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’.
Wimbo wa msanii huyo unaokosoa mambo mbalimbali ulipigwa marufuku na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), kabla ya Rais John Magufuli kutoa kauli ya kutaka uendelee kupigwa sambamba na msanii huyo kuachwa huru, ikiwa ni saa 24 tangu akamatwe na polisi kutokana na mashairi ya wimbo huo.
Kauli ya JK
Wakati hayo yakiendelea, Kikwete alizungumzia ujio wake bungeni na kubainisha kuwa sasa ni zamu yake kumuunga mkono mkewe kwa sababu wakati akiwa Rais, Mama Salma alimuunga mkono.
“Leo asubuhi nimeshuhudia kiapo cha mke wangu, Mheshimiwa Salma Kikwete kuwa mbunge wa kuteuliwa bungeni mjini Dodoma. Ni zamu yangu kumuunga mkono,” alinukuliwa Kikwete katika akaunti yake ya Twitter.
Mama Salma ambaye ni Mwenyekiti wa WAMA, alipotakiwa kueleza sababu za Rais Kikwete kushangiliwa, alisema: “Inaashiria kuwa Tanzania ni moja.
“Nashukuru wabunge kwa kunipokea vizuri, naamini tutafanya kazi nzuri kwa kushirikiana, shangwe na vigelegele vya leo (jana) vinaonesha Tanzania ni moja kwa kuwa zimetoka pande zote.”
Kauli za wabunge
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema shangwe hizo zinaashiria kuwa wabunge wamewakilisha wananchi wao kutoa hisia zao kwa Serikali ya Awamu ya Tano, ijue kwamba watu wanakumbuka walikotoka.
‘’Ile ilikuwa salamu kwa Magufuli, tunamkumbuka Kikwete, ambaye aliacha uchumi mzuri, mishahara ilikuwa inalipwa kwa wakati, watumishi walikuwa wanapanda vyeo, lakini sasa mambo yamekuwa ya hovyo kiwango chake aliyemwachia amekishusha,” alisema Msigwa.
Alisema Magufuli amedidimiza demokrasia, hafuati taratibu za bajeti ananunua ndege bila Bunge kuidhinisha, amehamia Dodoma bila Bunge kuidhinisha, hivyo ni lazima Bunge linalobanwa lioneshe hisia.
“Tumemkumbuka sana pamoja na kwamba hakuwa mzuri kihivyo, lakini ukimlinganisha na Magufuli anamwacha mbali mno, tulikuwa tunamtumia salamu kwamba Magufuli Watanzania waliingia ‘choo cha kike’, mambo ya hovyo sasa,” alisema Msigwa.
Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) alisema Kikwete alishangiliwa kutokana na namna ya uongozi wake, hivyo Watanzania wengi wamemkumbuka, kwani alikuwa Rais mchangamfu kwa watu wake, alipenda kupokea ushauri hata kama anatukanwa.
“Tuna kila sababu ya kumkumbuka Kikwete na kumshangilia, ndiyo maana mliona pande zote zilishangilia, hivi ndivyo wananchi walivyo, kwani sisi tunawakilisha wananchi na tulichoonesha ndizo hisia za Watanzania wengi,” alisema Bulaya.
Alieleza kipindi cha Kikwete vyama vya siasa vilikuwa na uhuru wa kufanya kazi zao kwa mujibu wa sharia, alikuwa anapambana na ufisadi kwa kuruhusu watu kuainisha maeneo yenye ubadhirifu, lakini sasa kila kitu kimeminywa
Alisema: “Kikwete tunamkumbuka kwa kweli, japokuwa hakuwa mkamilifu kwa asilimia 100 lakini ukimlinganisha na Magufuli hata ukiwaweka hapo Watanzania wengi watamchangua yeye, tunakumbuka uhuru wa kujieleza, uhuru wa Bunge na vyombo vya habari, uchumi unayumba yaani hakuna kuzuri.
“Napata shida mno mtu akisema Serikali inapambana na ufisadi wakati haitaki wananchi waeleze maeneo yenye ubadhirifu, akitokea mtu kueleza anaonekana adui wa Serikali, Kikwete alijitahidi kuacha watu wamwoneshe mafisadi na aliwawajibisha kupitia Bunge.”
Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema) alisema kitendo cha kumshangilia Kikwete kina tafsiri nyingi, lakini Serikali inataka kuendesha nchi kibabe, japokuwa wananchi wanapinga.
Kikwete hakuingilia Bunge, aliliacha lifanye kazi yake, hakuwa anasimama kutetea viongozi wanapotakiwa kuwajibishwa kama inavyotokea sasa katika Serikali.
“Viongozi awamu hii wakitaka kuwajibishwa Rais anasimama anatetea, Rais amekuwa akidhalilisha Bunge, Kikwete hakuyafanya hayo, aliruhusu demokrasia na uhuru utawale, sasa tunarudishwa nyuma miaka 50, hivyo wabunge walimshangilia kuonesha hisia zao kwake, japo hakuwa mkamilifu lakini alifanya mengi mazuri,” alisema Peneza.
Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta (CCM) alisema wabunge wamemkumbuka Kikwete kwa kazi nzuri aliyofanya wakati akiwa Rais lakini pia walishangilia kwa kuwa wengi hawajamwona siku nyingi.
“Nimemkumbuka kwa kutujengea barabara inayounganisha Tabora na mikoa mingine hali inayotusaidia kusafiri kirahisi lakini pia wabunge wengine huenda hawajamwona kiongozi wao aliyeongoza kwa miaka 10 hivi karibuni, ndiyo maana walimshangilia,” alisema Sitta
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alisema Kikwete anakumbukwa kwa mambo mengi mazuri, ukiwamo uhuru kwa vyama vya siasa kufanya kazi zao na kukaa kuzungumza nao.
Bunge lilikuwa huru kufanya kazi zake tofauti na sasa, ambapo linaminywa kufanya kazi zake, kwani kamati nyingi zinapangiwa kazi za kufanya haziko huru ndiyo maana baadhi ya wenyeviti wamejiuzulu.
“Kikwete alishangiliwa kwa mapenzi ya dhati na watu wamekumbuka uhuru ambao alikuwa anautoa na sasa umeminywa, biashara haziendi, uchumi unadidimia, wabunge hawafanyi kazi zao kama inavyotakiwa vitu vingi havieleweki,” alisema Waitara na kuongeza:
“Serikali ya Kikwete ilikuwa haina ubaguzi, mtu yeyote hata kama ni rafiki yake akiharibu anatolewa, lakini Serikali hii kuna mtu ameghushi vyeti anatumia jina la mtu mwingine, lakini Magufuli anaambiwa na anasimama kumtetea hadharani, ni lazima watu tumkumbuke Kikwete.”