NI katika mkutano wa waandishi wa habari katika Umoja wa Mataifa ulioandaliwa na Korea Kaskazini, ndipo unapoweza kumsikia mwanadiplomasia akiwatakia wanahabari sikukuu njema ya mwisho wa wiki halafu kutoa onyo la vita ya kinyuklia.
Katika miongo ya karibuni Korea Kaskazini imekuwa ikitoa vitisho vya mara kwa mara juu ya kuzuka kwa vita baina yake na Marekani, lakini utawala wa Rais Donald Trump ulitangaza kumalizika kwa zama za sera ya uvumilivu dhidi ya Pyongyang. Balozi mdogo wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa, Kim In Ryong aliitisha mkutano wa haraka wa waandishi wa habari jijini New York.
Mkutano huo uliandaliwa masaa kadhaa baada ya Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence kutembelea eneo lisiloruhusiwa shughuli za kijeshi katika mpaka wa Korea Kaskazini na Kusini. Pence alionya kwamba Korea Kaskazini isitake kuijaribu nchi yake “au nguvu za majeshi yetu.”
Huko New York, Korea Kaskazini ilirusha moto wa maneno. Balozi huyo alilaani kuongezeka kwa uwepo wa majeshi ya Marekani katika bahari karibu na peninsula ya Korea, pamoja na shambulizi la kombora lililofanywa dhidi ya Syria.
Kim alisema, “Hii imeleta hali ya hatari ambayo inaweza kusababisha vita ya kinyuklia kuibuka muda wowote katika peninsula na inatishia kupotea kwa amani na usalama wa dunia.”
Wakati waandishi katika Umoja wa Mataifa wamewahi kusikia lugha kama hiyo kutoka kwa Korea Kaskazini, maneno yaliyotolewa juziJumatatu yalikuwa ni makali zaidi.
Akisoma taarifa iliyoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari, alisema, “Marekani inataka kuharibu amani na ustawi wa dunia kwa kufanya mambo ya kihuni kama kufanya uvamizi wa taifa huru ni jambo jema ambalo lina lengo la kulinda ustawi wa ulimwengu na inajaribu kufanya hivyo katika peninsula ya Korea pia.”
Kim alisema kuwa nchi yake ipo tayari kuchukua hatua dhidi ya hali yoyote ya kivita kutoka kwa Marekani. Shambulizi lolote la makombora au nyuklia litakalofanywa na Marekani litajibiwa kwa nguvu ile ile,” alisema.
Ni wazi kwamba Umoja wa Mataifa una wasiwasi. Msemaji wake Stephane Durarric aliwaambia waandishi wa habari, “Tunasikitishwa na kuongezeka kwa hali ya wasiwasi ambayo tunaishuhudia katika peninsula ya Korea. Tunazitaka pande zote kutumia njia za kidiplomasia kumaliza tatizo hili.”
Korea Kaskazini ilifanya jaribio la kombora ambalo lilishindwa mwisho wa wiki hii. Dujarric alisema, “Nadhani jaribio la karibuni kabisa ambalo limefanyika mwisho wa wiki hii linatia wasiwasi. Tunaitaka Korea Kaskazini kuchukua hatua zote muhimu ili kutuliza hali ya mambo na kurudi kwenye meza ya mazungumzo ya kuachana na mpango wake wa kutafuta silaha za kinyuklia.”
Korea Kaskazini imekasirishwa kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaitisha kikao baadae mwezi huu kuzungumzia suala hilo, kikao ambacho kitaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson.