Msemaji Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Ally Saleh jana alisusa kuendelea kusoma hotuba yake kwa madai kuwa hakuna uhuru wa kujieleza katika chombo hicho cha kutunga sheria.
Saleh alikatiza hotuba hiyo, baada ya kutakiwa kufuta kauli iliyohoji uhalali wa Dk. Ali Mohammed Shein kukalia kiti cha Rais wa Zanzibar.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali( AG), George Masaju alisema maneno yaliyotamkwa na Saleh hayapo katika uhalisia.
Masaju alisema Saleh anapaswa kurekebisha kauli yake kwa sababu Rais Dk. Shein alishinda uchaguzi mkuu uhalali.
Kufuatia ushauri wa AG, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Hassan Zungu alisema maneno yaliyomo katika hotuba ya upinzani yaliyosomwa na mbunge Saleh ni lazima ayatoe kwa sababu siyo maneno sahihi na hayapo katika uhalisia.
“Kwa hiyo maneno katika ukurasa wa tatu, kwenye namba tatu inatoka, kwa Dk. Shein inatoka kwa sababu alichaguliwa kihalali, ukurasa wanne wote," alisema Zungu.
Hata hivyo Mbunge Saleh aliamua kuondoka bila ya kuendelea kusoma hotuba hiyo na kusema kuwa uhuru katika bunge hauko kiasi cha kutosha.
Mbali na kuhoji uhalali wa Rais wa Zanzibar, wakati akisoma hotuba hiyo Saleh alidai wizara zinakiona cha moto, mawaziri wamebanwa mbavu na kwamba muungano siyo ajenda ya awamu ya serikali ya awamu ya tano kutokana na matendo ambayo yanatokea.
Alisema endapo hali hiyo itaendelea basi "kidagaa kitamuozea mtu mkononi na maiti atampakata yeye."
Mara baada ya kusoma sehemu hizo katika hotuba yake, ndipo Mwanasheria Mkuu Masaju aliposimama na kutoa taarifa na kusema kuwa Saleh anatumia maneno ambayo ni makali.
Masaju alisema Saleh anapaswa kurekebisha kauli kwa sababu hakuna wizara iliyokiona cha moto wala waziri aliyebanwa mbavu, pia Rais Dk. Shein alishinda uchaguzi mkuu kwa uhalali.
Kauli hiyo ya Masaju ilizua tafrani bungeni hali iliyosababisha baadhi ya wabunge upinzani kusimama na kuomba taarifa.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema Mwanasheria Mkuu Masaju anapoteza muda kwa kuwa anazungumzia masuala ambayo hayapo kikanuni.
Naye Mbunge wa Iringa mjini (Chadema), Peter Msigwa alisema uhuru wa kambi ya upinzani upo kikatiba.
Alisedma bunge linaendeshwa kwa kanuni hivyo walio wachache wasikilizwe na walio wengi wanapswa kutoa maamuzi.
“Sasa Serikali hata sisi tuliowachache tunavyotoa maoni na mawazo tunazuiwa, hivi utamaduni wa bunge hili ni upi? AG badala ya kuisaidia Serikali ili inyooke amekuwa mtetezi, na bado anapotosha hapa," alisema Msigwa.
"Sisi ni upinzani na ndiyo kazi yetu, sasa kama kila kitu tunachoandika tunapingwa, mnataka tufanyeje? Hatujaja hapa kuwasikiliza nyie.”