Wabunge wa CCM Wamkaba Koo Waziri wa Magufuli...Waunga na na Upinzani Kudai Katiba Mpya...!!!


Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amebanwa na wabunge kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.

Jana ilikuwa mara ya kwanza kwa Profesa Kabudi kufika mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, akiwa katika nafasi ya uwaziri baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo, baada ya Dk Harrison Mwakyembe kuhamishiwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Profesa Kabudi alisema hajakutana na viongozi wake kuzungumzia suala la Katiba Mpya, ingawa anajua mambo mengine kuhusu mchakato huo ambao wakati wa maandalizi yake, alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Wabunge wa CCM walikuwa wa kwanza kuibua hoja hiyo jana wakisema Katiba Mpya ni sehemu ya ilani ya uchaguzi ya chama chao.

Mbunge wa Bahi (CCM), Omari Badwel alimtaka waziri huyo aseme ni lini hasa mchakato huo utaendelea na Watanzania watarajie kuipata lini Katiba hiyo.

Mbunge huyo alisema mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 hayaonyeshi ni mahali gani na kifungu kipi kitakachotumika kwa ajili ya kusaidia mchakato wa katiba ikiwamo upigaji wa kura ya maoni.

“Hata humu sijaona kama kuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya, najiuliza ina maana si kipaumbele au mmesahau kuwa hata ilani ya uchaguzi ya CCM imetaja suala hilo?” alihoji Badwel.

Mbunge wa Malindi (CUF), Ali Saleh alisisitiza kutozimwa kwa suala hilo kwa kuwa ni muhimu sasa na akahoji kwa nini linachukua muda mrefu kukamilika.

Saleh alisema inashangaza kuona mchakato huo ukipelekwa kwa mwendo wa kusuasua licha ya kuwa fedha nyingi za walipakodi zilishatumika.

Mbunge huyo ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alilalamika kuwa suala la Katiba Mpya limezimwa, akataka Serikali kusoma alama za nyakati kuwa huu ndiyo wakati wake.

Hata hivyo, Profesa Kabudi alisema ana muda mfupi katika wizara hiyo na kwamba, hajapata muda wa kukutana na mabosi wake akiwamo Waziri Mkuu, ili wazungumzie suala la Katiba Mpya.

“Najua nia yenu njema, ninalichukua jambo hili na nitahakikisha nalifikisha kwa wakuu wangu yaani Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na kulifikisha kwenye Baraza la Mawaziri,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema mchakato huo unahitaji umakini mkubwa hivyo atafanya kazi kulingana na utaratibu wa kisheria ili liwe na mwanzo na mwisho mzuri.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad