WAKATI Chadema Wakimchukia Magufuli..Mwasisi wa Chadema Aibuka na Kumshushia Sifa Kedekede..Afungulka Pia Hatma ya Lowassa Ndani ya Chadema...!!!!


MWASISI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei, ameeleza kufurahishwa kwake na mwenendo wa uongozi wa kushtukiza na utekelezaji wa sera za Chadema unaofanywa na Rais John Magufuli. RAI linaripoti.

Tangu alipoingia madarakani Novemba 5, mwaka 2015, Rais Magufuli amekuwa akifanya ziara za kushtukiza katika idara na taasisi mbalimbali za umma, huku baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wakidai kuwa anatekeleza Ilani ya Chadema.

Katika mazungumzo yake na RAI, Mzee Mtei ambaye pia alikuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alisema Rais Magufuli amewafungulia njia wapinzani, hivyo wanamsubiri kwa hamu katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“Tena nikuambie kwamba kama kuna jambo ambalo tunajivunia sisi ni pale ambapo serikali inatekeleza sera ya chama changu ambacho nilikianzisha. Hili linanipa furaha, pamoja na udhaifu uliopo ndani ya serikali ya Awamu ya Tano. Ukiangalia elimu, afya, barabara, kufufua reli, viwanda pamoja na mambo kadha wa kadha, najivunia kwamba chama changu ni chama bunifu, kila siku tunabuni mambo mapya kulingana na mabadiliko ya teknolojia.

“Chadema kinasikiliza maoni ya Watanzania, bila kujali ukanda wala kabila. Chadema ni wapenda amani, tutaendelea kumwenzi hayati Baba wa Taifa hili na mwaasisi wetu aliyetukomboa mikononi mwa wakoloni. Alionyesha uzalendo na siyo chama. Hakutaka madaraka, alitanguliza uzalendo wake, tofauti na viongozi wa chama tawala ambao mawazo yao yametawaliwa na uongozi na siyo uzalendo wa kuipenda nchi yao. Hili ni jinamzi linalolitafuna Taifa hili.

“Sasa hivi mimi siwezi kupambana kwenye majukwaa ya siasa, ila nitaendelea kuwaonya viongozi wa chama changu kwa kutumia  mitandao ya kijamii whatAspp na mitandao  mingine, ili waendelee kuyaenzi yale yaliyomema ya kulijenga Taifa hili,” alisema.

HALI YA KISIASA

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Mzee Mtei alisema hali inabadilika badilika kutokana na mtindo wa Rais Magufuli anaoutumia kuongoza nchi.

“Hivi sasa nchi inaongozwa na Rais ambaye anafanya mambo yake kwa kushtukiza shutukiza na sisi tunamwangalia tu, tuone atafika wapi. Pili nchi haiwezi kuendeshwa kwa mtindo wa namna hii, nchi inatakiwa kuendeshwa kwa kufuata sheria na Katiba.

UJIO WA LOWASSA

Aidha, akizungumzia ujio wa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ndani ya Chadema na kupewa nafasi ya kukiongoza chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Mzee Mtei alisema ujio huo ulionyesha ni jinsi gani Watanzania, pamoja makada wa walioko ndani ya CCM walivyochoshwa na mambo ambayo yaendelea ndani ya Serikali.

“Lowassa alikuja kuunga mkono, ili kuleta ukombozi wa Watanzania ambao bado wako kwenye giza nene na hawajui wanakwenda wapi, mbali kuwa nchi yao imesheheni rasilimali nyingi na ardhi zenye rutuba.

“Lowassa pia alikuja ili atusaidie kuchukua nchi, lakini niwaambie kwamba bado tutaendelea kuwa na Lowassa hatutaweza kumtupa. Alileta mabadiliko makubwa sana aliwachangamsha vijana, aliweza kuamsha ari mpya.

SLAA ALINIVUNJIA HESHIMA
Akizungumzia uamuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa kuondoka ndani ya chama hicho katika kipindi cha mwisho cha mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2015, Mzee Mtei alisema hilo ni jambo lililomsitikisha sana.

“Kwanza aliondoka kipindi ambacho tuko kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Binafsi Dk. Slaa ni rafiki yangu wa karibu sana, kwa jina lingine namfananisha kama kijana wangu, kabla ya kuondoka kwake nilimsihi sana lakini hakunisikia, nilimwandikia ujumbe mbalimbali kumtaka anieleze juu ya kuachana kwake na siasa, hakunijibu. Nikamwandika barua, hakujibu nikajisikia vibaya sana. Sikutegemea kama angenifanyia hivyo.

“Ukimya wake wa kutonijibu niliona mimi kama rafiki yake msiri wake, tena mtu mzima, moja kwa moja nikaona kama amenivunjia heshima.

“Siwezi kumsahau kwani alikuwa chachu kwa vyama vya upinzini, alikuwa mwanamapinduzi wa kweli, bila kujali ni nani anapambana nae. Kwenye siasa alikuwa akiisema Serikali bila kuogopa, tena kwa hoja. Alikuwa mtu ambaye aliipenda nchi yake, alikuwa akikisema chama tawala kwa kuwataja mafisadi waliokuwa wanatafuna nchi bila kuwaangalia usoni, tena kwa ushahidi. Pia alikuwa akishirikiana na viongozi wa wake katika kila hali, ni mtu asiyependa kuonewa wala kuwaonea wengine.

“Ila nina imani Dk Slaa bado ni mwanaChadema na ataendelea kuwa mwanamapinduzi, hata ukiangalia siyo yeye pekee yake aliyeondoka, waliondoka wengi wazuri pia, akina Zitto Kabwe na wengine, lakini heshima yake inabaki pale ambapo alibaki bila kujiunga na chama kingine. Huo ndiyo uzalendo wa kweli, hata akija nchini nitamwita, maana najua hatokataa mwito wangu,” alisema.

MWELEKEO WA CHADEMA 2020

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020, Mzee Mtei alisema hivi sasa chama hicho kimejipanga, kwa kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kilishiriki na kufanya vizuri kuanzia ngazi za udiwani, ubunge na urais, lakini CCM kwa uzoefu wao waliiba kura kwa kutumia nguvu ya dola.

“Kwa kuwa Chadema ni chama makini na kinaongozwa na watu ambao ni wasomi, wenye maadili, hatukutaka kwenda kufanya maandamano. Pili, kwa kulinda heshima ya Watanzania waliotuamini, hatukutaka kufanya mikutano ya kupinga matokeo ya urais. Tatu, Watanzania walio wengi, hawakuwa tayari kwa mabadiliko uongozi wa juu kwa kuhofia huenda ingeleta vita endapo mgombea wa Chadema, Edward Lowassa angetangazwa kuwa rais.

“Ila uchaguzi ujao mwaka 2020, Chadema tutashinda kiti cha urais kwa kishindo kwani tumejipanga, hatutaogopa chochote siwezi kuweka wazi mkakati wetu tuliyopanga.

“Kwa sababu tunaona pia kijana wetu Zitto Kabwe amedhamiria kuongeza nguvu, jambo ambalo ni jema na linaonesha jinsi gani vijana wangu niliowalea, wamekomaa kisiasa. Zitto bado ni mwanachadema, kuihama Chadema haimzuii Zitto kuipenda Chadema. Bado ana mapenzi ya dhati, kwani ndiyo chama ambacho kilimleta na kilimpa umaarufu kwenye nyanja za kisiasa ndani na hata nje ya Tanzania.

Naamini muungano wa UKAWA utasaidia kuimarisha upinzani kuingia madarakani mwaka 2020, pia utasaidia kuua nguvu za chama tawala, kwani ndicho kilichokuwa kikiwagharimu na kushindwa kufanikiwa kutokana na mgawanyiko wa upinzani. Umoja ni muhimu sana katika kudai haki na kujenga Taifa, hasa kwa nchi kama Tanzania ambayo haijawahi kutawaliwa na vyama vya upinzani.

Licha ya muungano huo, Mzee Mtei anasema bado hawajaweka mikakati ya kuainisha jina la mgombea urais katika uchaguzi wa 2020.

“Naweza nikasema ni sahihi au la, lakini Lowassa bado ni wa kwetu, siwezi kuiweka wazi mikakati ya chama kwani maamuzi yatakuja wakati ukifika, kwa sasa bado ni mapema mno na kama mnavyojua, Chadema ndiyo chama pekee nchini kilichosheheni vichwa vilivyojaa ubunifu na sera ambazo hazikopiki.

Pili Chadema ni chama ambacho kinasikiliza maoni ya Watanzania na kuyafanyia kazi kulingana na mabadiliko hali ya kisiasa katika nchi kwa wakati husika.

Tatu tutaangalia ni kwa namna gani tutaboresha, ili kuchukua nchi mwaka 2020 kwa kushirikiana na vijana wetu walioko ndani ya chama. Na imani yetu kubwa ni kuchukua nchi mwaka 2020, kwani sasa wananchi wako tayari kwa maamuzi yoyote na kuna kila dalili, hata ukisema uchaguzi ufanyike leo, lazima tuchukue nchi. Watanzania wa leo sio wale wa jana. Ndio maana nasema Tanzania mpya inakuja.



SERIKALI YA AWAMU YA TANO

Aidha, akizungumzia mwenendo wa Serikali ya awamu ya Tano, Mzee Mtei anasema kiujumla Rais Magufuli ni kiongozi mzuri kwa kiasi, ila anadhani Watanzania wataamua kwa kuwa ni mtu wa kufanya mambo kwa kushtukiza.

“Amekuwa akifanya maamuzi yake kwa matukio na siyo kuwasikiliza Watanzania wanasemaje, nini mahitaji ya watu wake, hivyo sisi kama wapinzani tunaangalia tu tuone ataifikisha wapi nchi kwa miaka mitano. Sasa hivi tayari amebakisha miaka mitatu tu,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, alisema ni kosa kubwa kumfananisha Mwalimu Nyerere na Magufuli kwa kuwa Nyerere alikuwa analipigania Taifa kutoka kwenye makucha ya wakoloni.

“Huwezi kumfananisha na wanasiasa vijana, tena wanaoliharibu Taifa, Mwalimu Nyerere alikuwa anapigania haki na kuikomboa nchi mikononi mwa wakoloni, leo hii watu kumfananisha na wanasiasa ni jambo la kusikitisha sana,” alisema.

Anasema sera ya kufufua viwanda ni sera ambayo haitekelezeki kwa kuwa jukumu hilo ni jambo linalohitaji maandalizi makubwa.

“Kwanza lazima uwaandae wananchi unaowaongoza, pia kushirikiana na pande zote pili bila kuangalia itikadi ya vyama, kuandaa mazingira ya wawekezaji wa ndani na wa nje, upatikanaji wa malighafi pamoja watalaamu wa masuala kiuchumi na viwanda. Tatu, lazima uandae au kutenga ardhi kwa ajili ya viwanda  kwani hakuna njia rahisi bila kufuata hatua zote.

Aidha, alisema uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta mikutano ya kisiasa hadi 2020, ni jambo ambalo limewafungua macho wapinzani kwa kutumia mitandao ya kijamii kufanya siasa za kimyakimya.

“Ni utashi wa kiongozi aliyeko madarakani na chama chake, na sisi kwetu ni fursa, ametupa mwanga wa kuona mbali zaidi. Pili amevisaidia vyama vya upinzani kuongeza ubunifu, kubadilisha namna ya kufanya siasa na kwamba siyo lazima kufanya siasa kwenye majukwaa.

Ametupa fursa nyingine nzuri ya kufanya siasa badala kutumia gharama kubwa kuandaa mikutano na watu, tunatumia mitandao ya kijamii kuwaeleza Watanzania na tumegundua njia hii ni bora zaidi, kwani tumeweza kuwafika idadi kubwa ya vijana, wamama pamoja na wababa.

“Sasa hivi ukirusha kitu kwenye mitandao ya kijamii baada ya dakika tano tayari unapokea zaidi ya komenti za watu 1000 kutoka mikoa yote Tanzania na hata nje ya nchi, imetusaidia kufanya siasa za kimya kimya, kuliko kuandaa mkutano ya hadhara. Binafsi na namshukuru kwa utashi wake ametufungua macho na ufahamu zaidi. Siasa hazizuiliki kamwe,” alisema. 

Credit - Rai

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad