KUNDI la majambazi 15 wakiwa na silaha za jadi na milipuko ya baruti limevamia kitongoji kisha kubaka wanawake, kujeruhi, na kupora fedha na madini usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo lililotokea katika Kitongoji cha Machinjioni kilichopo katika Kijiji cha Mugusu wilayani Geita na lilichukua takriban saa moja.
Majambazi hao walikuwa na nondo, mapanga, fimbo na milipuko ya baruti.
Katika tukio hilo, wanawake wawili walibakwa na watu tisa kujeruhiwa kwa silaha hizo, imeelezwa na kwamba watatu kati yao, akiwamo Mwenyekiti wa kitongoji, Abdul Hamza, walilazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Geita.
Mbali na kubaka na kujeruhi, watu hao pia walipora kiasi cha fedha na gramu 30 za dhahabu, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. milioni tano kisha kutokomea kusikojulikana.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limepeleka makachero na askari wa kitengo maalum cha kupambana na unyanga’anyi wa kutumia silaha ili kuwasaka majambazi hao.
Jeshi hilo pia limewataka wahusika wa vitendo hivyo kujisalimisha kabla ya kukamatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Lodson Mponjoli, aliyetembelea eneo la tukio, alisema kitendo hicho hakikubaliki na msako mkali umeanza.
Kamanda Mponjoli alisema kundi la majambazi hao lilivamia Kitongoji cha Machinjio saa sita usiku wa juzi na kuwaweka chini ya ulinzi kwa karibu saa moja baadhi ya wakazi wa eneo hilo.
Katika uvamizi huo, Kamanda Mponjoli alisema, watuhumiwa walivunja vibanda vya maduka na nyumba za makazi kisha kupora mali zikiwamo simu za mkononi, dhahabu na fedha taslimu vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. milioni tano.
Kamanda Mponjoli alisema wakati wa kutekeleza uhalifu huo, watuhumiwa waliwajeruhi wananchi.
Imeelezwa kuwa ili kutekeleza azma yao, majambazi hao walilipua baruti zilizotengenezwa kienyeji kwa lengo la kuwatia hofu majirani waogope kufika kutoa msaada.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema watuhumiwa wa uhalifu huo ni vijana wenye umri wa miaka kati ya 20 na 30 na kwamba walitumia mapanga na fimbo kuwajeruhi.
Marco Mjema na mwenyekiti wa Kitongoji cha Mugusu, Emmanuel Mapalala, walisema katika tukio hilo, majambazi hao waliwabaka wanawake wawili.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo pamoja na Hamza ni Damas Josiah na Sele Seif ambao wamelazwa pia katika Hospitali ya Rufani ya mkoa wa Geita.
Wengine ni Joram Abel, Ibrahim Daud, Sweetbert Nicholaus na Masinde Thomas ambao walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka pamoja na wanawake wawili waliotendewa ukatili wa kijinsia (majina tunayahifadhi).