Kambi ya Upinzani bungeni, inayohusika na Ofisi ya Makamu wa Rais, imesema kutokana na ukata ofisi hiyo ilalazimika kukopa ili kumhudumia Makamu wa Rais.
Awali, Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria iliungana na upinzani kutoa kilio cha ofisi ya Makamu wa Rais kukabiliwa na ukata kutokana na kutengewa fedha kidogo, hali ambayo imeelezwa kuwa kwa kiasi kikubwa inaathiri utekelezaji wa majukumu yake.
Kamati hiyo ilitoa kilio hicho wakati ikiwasilisha maoni kuhusu bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa fedha 2017/18, iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Nchi katika ofisi hiyo, January Makamba.
“Mwenendo wa bajeti unaonyesha kwamba ukomo wa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais umekuwa ukishuka tangu mwaka wa fedha 2015/2016 kwa kiasi kikubwa,” alisema mjumbe wa kamati hiyo, Joseph Mhagama alipokuwa akisoma taarifa hiyo.
Alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 ukomo wa bajeti ulishuka kwa wastani wa Sh17 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16.
Wakati kamati ikisema hayo, Kambi ya Upinzani ilisema suala la kuipunguzia bajeti Ofisi ya Makamu wa Rais halikubaliki.
Katika hotuba yake ambayo hata hivyo, haikusomwa bungeni baada ya waziri kivuli wa Muungano aliyekuwa anaisoma, Ally Salehe kususa alipolazimishwa kuhariri baadhi ya maneno, alisema kutokana na upungufu wa bajeti, ofisi hiyo ililazimika kukopa ili kumhudumia Makamu wa Rais.