Watu 53 wanaosadikiwa kuwa wavuvi wamenusurika kifo baada ya boti yao kukumbwa na dhoruba na kuzama baharini eneo la Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Hasina Ramadhan Tawfiq alisema boti hiyo inafahamika kwa jina la Advantage na watu hao waliokolewa, na baada ya matibabu katika hospitali za Tumbatu na Kivunge waliruhusiwa kurejea makwao.
Hasina alisema taarifa za tukio hilo walizipata juzi jioni baada ya kuokolewa kwa mmoja wao na meli ya Azam Link iliyokuwa ikitokea Pemba kwenda Unguja na kuwa boti hiyo ilizama saa nne asubuhi. Kamanda huyo alisema jitihada za uokoaji zilifanywa na vikosi vya KMKM, ZMA na Polisi.
Mvuvi aliyeokolewa, Khatib Khamis ambaye ni mkazi wa Mtoni alisema chanzo cha tukio hilo ni upepo mkali ulioambatana na mawimbi yaliyosababisha chombo chao kupinduka. Alisema kabla ya tukio hilo walikuwa wanatokea Mtoni kuelekea Kisiwa cha Tumbatu kuvua.