Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema viongozi waandamizi wa chama cha wananchi (CUF) ndiyo walihusika na tukio la kulipua bomu katika nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar baada ya kufanyika uchaguzi mkuu
Mhe. Masauni alieleza hayo Bungeni Jijini Dodoma jana pindi alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Gandu kupitia tiketi ya (CUF) visiwani Pemba, Mhe. Othuman Omary Hajji alipotaka kujua kwanini mpaka leo hajizachukuliwa hatua stahiki kwa wafuasi wa CCM waliochoma nyumba za wanachama wa CUF huko visiwani Tumbatu, huku akidai serikali iliyopo madarakani siyo halali ni haramu kwa kuwa Jeshi la Polisi lilichangia kumuweka madarakani Dkt. Ali Mohamed Shein.
"Ni kweli baada ya uchaguzi mkuu baadhi ya vyama vya upinzani ikiwemo chake, viongozi walijitokeza kuhamasisha wananchi kufanya mambo yanayokiuka sheria za nchi yetu.
"Kuna matukio mbalimbali yalijitokeza ikiwemo kuchomwa moto nyumba, kuchoma mashamba, kurusha mabomu ikiwemo nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi wa Zanzibar ambayo kwa uchunguzi uliofanyika mpaka sasa, watu waliokamatwa kwa kuhusika urushaji bomu katika nyumba ya Kamishna ni viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF)". Alisema Masauni
Pamoja na hayo, Masauni alisema Jeshi la Polisi limeshakamilisha uchunguzi wake na jalada la mashtaka lipo kwa DPP muda wowote kuanzia sasa litapandishwa Mahakamani ili sheria ichukuliwe.