MAISHA ni vita bwana. Ili uweze kushinda, lazima upambane kweli. Wapo wanaoamini kuwa ‘kutusua’ kimaisha lazima uwe umesoma lakini huenda hiyo si siri pekee.
Ni kweli elimu inaweza kurahisisha lakini haimaanishi kuikosa ndio chanzo cha kufeli maisha. Kutambua kipaji ulichonacho na kukipigania ni njia nyingine rahisi ya kufanikiwa.
Maisha ya mwanamuziki, Ayo Balogun ‘Wizkid’ yamethibitisha kuwa kipaji kinaweza kukufanya uishi maisha ya kifahari nje ya elimu.
Kwa sasa Wizkid ni miongoni mwa wasanii maarufu Nigeria, Afrika na duniani kote, lakini linapokuja suala la elimu ni ‘kimeo’.
Elimu ilimshindaje?
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Wizkid hakuwa na bahati na elimu, ni muziki pekee ndio ‘uliomtoa’ na kumfanya kuwa hapo alipo.
Kwanza, alifukuzwa shule akiwa sekondari kutokana na kitendo chake cha kuiba mali za shule.
Siri ya kutimuliwa shule kwa kitendo hicho cha ‘Panya road’ ilifichuliwa na waliokuwa wanafunzi wenzake katika Shule ya Sekonadri ya Ijebu Ode Grammar.
Kwanini Olumide Adewale na Adetunji Adedokun-Fernandez ‘ Najia Child’ waliamua kuuweka wazi ukweli huo wa Wizkid?
Washikaji hao walikerwa na kitendo cha Wizkid kuchukua fedha na kushindwa kutokea kwenye ‘show’ waliyoiandaa.
Kuthibitisha kuwa elimu ilimkataa kabisa Wizkid, aliwahi kurudi darasani na kufika ngazi ya chuo kikuu lakini alichemsha kwa mara ya pili. Safari hii, sababu ilikuwa ni usumbufu kutoka kwa watu waliokuwa wakimuona staa!
“Nilikuwa chuo (Chuo Kikuu Leadcity) na niliacha nikiwa mwaka wa pili. Kabla ya kuacha, nilikuwa nafanya vizuri kwenye masomo na hata wazazi wangu walikubali hilo.
“Lakini muziki wangu ulipokuwa, sikuweza kutulia darasani kwa sababu watu walikuwa wakinizonga sana.
“Ilinichanganya na sijui kama nitapata chuo hapa Nigeria ambacho sitakuwa nikizongwa.
Kwa mujibu wa Wizkid, hali hiyo ilisababisha atemane kwanza na shule na kisha kuelekeza nguvu zake kwenye muziki.
Mwimbaji wa kwaya
Nyota huyo alizaliwa Julai 16, mwaka 1990 na alianza muziki akiwa na umri wa miaka 11. Kwa kuwa familia yake ilikuwa ni waumini wazuri wa Dini ya Kikiristo, Wizkid alikuwa akihudhuria kanisani na kuimba kwaya. Walikuwa na kikundi chao walichokipachika jina la Glorious Five.
Banky W ndiye aliyemtoa
Mwaka 2009, staa wa muziki nchini Nigeria, Banky alivutiwa na uwezo wake na ndipo alipomchukua na kumpa mkataba kwenye lebo yake ya Empire Mates Entertainment (E.M.E).
Wizkid aliweza kurekodi ngoma yake ya kwanza na iliyomtoa ya ‘Holla at Your Boy’. Baadaye ndipo alipoachia ‘Tease Me/Bad Guys’, ‘Don’t Dull’, ‘Love My Baby’, ‘Pakurumo’ na nyinginezo.
Kufikia mwaka 2010, tayari Wizkid mwenye umri wa miaka 27, alianza kupata umaarufu kwenye soko la muziki barani Afrika.
Kashfa kibao
Wizkid amekuwa akiteka vichwa vya habario za burudani kutokana na matukio yake ya ajabu. Itakumbukwa kuwa, wanafunzi wa Chuo Kikuu Lagos waliwahi kumfikisha kwenye vyombo vya sheria wakidai kudhulumiwa na Wizkid wakisema walimpa fedha ili atumbuize kwenye ‘party’ lakini hakufika.
Ni kipindi hicho pia Wizkid alikuwa akitajwa kumpachika mimba mwanafunzi wa Chuo Kikuu Legon kilichopo mjini Accra, Ghana.
Wizkid aliwahi kukataa kumpachika mimba mwanafunzi wa chuo, Sola Ogudugu na mara kadhaa msanii huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa hajui chochote kuhusu taarifa hizo.
Hata hivyo, baada ya Sola kujifungua Wizkid alianza kuuficha ukweli na kujikuta akianza kujiachia na mtoto wake kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa sasa dogo huyo aitwaye Boluwatife Balogun, ana umri wa miaka saba.
Hivi sasa Wizkid anatoka na mlimbwende mzaliwa wa Guinea anayeishi Marekani, Binta Diamond Diallo na tayari wamebahatika kupata mtoto mmoja anayeitwa Ayodeji Balogun a.k.a King Ayo.
Muziki umemtajirisha
Wikid ni mmoja kati ya wasanii wenye mafanikio makubwa Nigeria na amekuwa akifananishwa na Justin Bieber.
Mwaka 2015, jarida la Forbes la Marekani lilidai kuwa mwanamuziki huyo ameingiza Dola za Marekani milioni 11 (zaidi ya Sh bilioni 24 za Tanzania).
Pia, katika vyanzo vyake vya mapato, Wizkid anamiliki studio iitwayo Starboy Entertainment ambayo imekuwa ikifanya vizuri kwenye soko la muziki nchini Nigeria.
Nyota huyo anamiliki magari ya bei mbaya yakiwamo Porsche Panamera, Volkswagen, Mercedes 2012, Hyundai Sonata, BMW X6 na Bentley. Mbali na usafiri, pia ana bonge la nyumba mjini Lagos ambalo linatajwa kuwa na thamani ya Naira milioni 200 (zaidi ya Sh bilioni moja za Tanzania) na anayo nyingine mjini Los Angeles, Marekani.
Lakini pia, taarifa zinasema huwa analipwa si chini ya Naira milioni 5 kila anapofanya ‘shoo’.
Alishika nafasi ya tano ya wasanii matajiri Afrika katika orodha iliyotolewa na Fobes mwaka 2013.