Uongozi wa klabu ya Young Africas wamefunguka mazito baada ya mashabiki wa timu hiyo kulalamikia hatua ya uongozi huo kupeleka timu B vijana chini miaka 20 kuchuana na Kombaini ya majeshi siku ya jana.
Katika taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga amesema kulikuwa na dosari kadhaa katika kufikia makubaliano ya ushiriki wa mechi hiyo ya kirafiki katika kilele cha sherehe za Muungano zilizofanyikia huko Mjini Dodoma hasa upande wa stahiki ya timu hiyo pamoja na ukaribu wa ratiba za michuano ya nusu fainali za FA.
"Uamuzi wa kutokupeleka kikosi cha kwanza ni kwa maslahi mapana ya Yanga katika kufanya vizuri mashindano tunayoshiriki lakini pia kulikuwa na dosari kadhaa katika makubaliano ya ushiriki wa mechi hiyo hasa upande wa stahiki ya Yanga, upana wa kikosi, ukaribu wa mechi ya FA na ligi kuu pia". Alisema Sanga
Pamoja na hayo, Sanga amewaomba radhi mashabiki wote waliosikitishwa na uamuzi huo kwa namna moja ama nyingine huku akiwasii waendelee kuungana na kushikamana ili waweze kutwaa makombe wanayoshiriki kwa sasa.
Kwa upande mwingine, timu ya Yanga U20 iliweza kutoka sare ya bao 1-1 ambapo goli hilo la Yanga lilifungwa na Yusuph Mhilu kwenye dakika 52 ya mchezo.