WAKATI msanii wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, akiendelea kusaka faraja ya moyo kutokana na kudai kuwa amekuwa akikabiliana na vitisho, mama yake mzazi ameamua kuondoka nyumbani kwake akihofia kuuawa.
Nay aliingia kwenye mgogoro na serikali kutokana na wimbo wake wa Wapo uliosababisha ashikiliwe na jeshi la polisi pamoja na wimbo huo kufungiwa na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) lakini aliokolewa na kwa amri ya Rais John Magufuli.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Nay amesema pamoja na tamko la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, kutoka kwa rais, kuruhusu wimbo wake uchezwe kote, ameendelea kuwa na vitisho kila kukicha kutoka kwa watu asiowafamu.
“Ninaishi kwa mashaka makubwa, tangu nilipoachia wimbo huu, maana kumekuwa na mfululizo wa kupigiwa simu na meseji za watu wakinitishia maisha jambo ambalo limepelekea hadi mama yangu kuamua kuhama nyumbani kwangu na kurudi kwake.
“Kabla sijatoa wimbo huu nilikuwa naishi na mama nyumbani kwangu, lakini ameamua kuondoka kufuatia kutishiwa maisha kila kukicha, lakini baya zaidi vitisho hivyo vimenifanya mimi na mama kupishana mawazo ambapo ameniambia niachane na wimbo huo, tena ikiwezekana niachane na muziki ili nifanye biashara zingine jambo ambalo sijamkubalia.
“Nafikiri kutomkubalia kwangu dhahiri nahisi itakuwa ndicho kisa cha kuamua kuondoka na kurudi nyumbani kwake, napata tabu sana na wimbo huu, lakini naamini mimi ni mtu wa misimamao hivyo siwezi kuachana na muziki kisa vitisho.
“Katika maisha hakuna jambo rahisi hasa kama wewe ni mpambanaji, vitisho kama hivi sitaki kuvipatia nafasi ya kuniharibia maisha kwani mimi ninachokifanya ni kuwakilisha mawazo ya wazalendo wengi ambao imekuwa ni ngumu kila mmoja kufikisha maoni yake kwa jamii.
“Kuna watu wanadhani nilipoitwa na Mwakyembe nilienda kushikiwa akili ili nibadili muziki wangu lakini ukweli ni kwamba, kule alikuwa akinipa ushauri wa kawaida tu, hivyo hakuna jambo ambalo amenibadilisha kwenye muziki wangu na nitaendelea kupigania ninachokiamini ili nitimize ndoto yangu.
“Kifo kipo tu lakini wengi t u m e k u w a waoga wa kutangulia hasa ukifikilia jamii inayokuzunguka, Wapo imenikutanisha na watu nisiowafahamu, maana nakumbuka siku mbili nyuma zilizopita nilipigiwa simu na mtu nisiyemjua akidai anahitaji kufanya biashara na mimi hivyo nikaenda kuonana nae Ubungo.
“Huwezi kuamini ningekua muoga basi nisingemsikiliza maana baada ya kukutana alinitoa chemba na kuanza kunihusia juu ya kuachana na wimbo huo akidai watu wamejifanya kunichunia lakini hakuna anayefurahishwa, hivyo kama nataka amani iendelee basi niuache na kingine akaniamia niwe makini kwani kuna watu wana nia mbaya na mimi.
“Kusema kweli nimeshatishwa sana lakini watu wanachotakiwa kujua kama kifo kipo basi nitakufa kwa kuwatetea mamilioni ya mashabiki zangu, ila suala la kushikiwa akili au kubadilishwa gia yangu hapa halina nafasi,” anasema Nay.
Ikumbukwe kwamba mwishoni mwa wiki iliyopita Nay baada ya kutoka Dodoma, alikoenda kuitikia wito wa waziri Mwakyembe, alisema amefarijika kwa namna moja au nyingine hasa baada ya kukutana, kwani walipata muda wa kuketi na kuzungumza mambo mengi juu ya sanaa ya muziki.
Huku akimtaka kuwa makini na tunzi zake kwani zimekuwa na mfululizo wa maneno ya kuwagusa watu moja kwa moja hivyo awe makini kwani kuna wengine huwa si wavumilivu kwani asipojiahadhali wanaweza kuja kumdhuru kwa namna moja au nyingine.