A - Z y Jinsi Ajali ya Basi Arusha Ilivyopoteza Ndoto za Wanafunzi 33..Ajali Ilikuwa Hivi Tofauti na Inavyoripotiwa..!!!


SIKU ya Mei 6 mwaka huu (2017) ni kati siku zitakazokumbukwa na wakazi Arusha na Tanzania kwa ujumla wake kwa muda mrefu.

Siku hii imeacha kumbukumbu mbaya kufuatia ajali mbaya ya gari iliyopoteza uhai wa wanafunzi 33 wa shule ya mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vicent iliyopo eneo la Kwa Mrombo katika Jiji  la Arusha.

Pamoja na wanafunzi hao 33 ambao wote ni wa darasa la saba pia katika ajali hiyo maisha ya walimu wawili wa shule hiyo, Innocent Pappian na Julius Mollel na dereva Dismas Kessy, walipoteza maisha hivyo kufanya idadi ya waliofariki katika ajali kufikia watu 36.

Walionusurika katika ajali hiyo ni wanafunzi wawili wa kike ambao hadi usiku wa kuamkia leo (Mei 7, 2017) walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru ambao hata hivyo majina yao hayakuweza kupatikana mara moja.

Ajali hiyo mbaya ambayo itabaki katika kumbukumbu za ajali mbaya kuwahi kutokea mkoani Arusha na nchini ilitokea saa 2.30 asubuhi (Mei 6) katika kijiji cha Rhotia baada ya gari hilo kuacha barabara na kutumbukia katika korongo la mto Marera, lenye urefu unaokadiriwa kuwa kati ya mita 20 hadi 25.

Wanafunzi hao waliokuwa wakitumia usafiri wa basi la shule aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili  T 872 BYS  walikuwa safarini kuelekea wilayani Karatu, kushiriki mitihani ya ujirani mwema na wenzao wa shule ya Tumaini Academy iliyopo mjini Karatu.

Basi hilo lilikuwa kati ya mabasi matatu ya shule hiyo yaliyokuwa yameongozana na taarifa  kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa gari iliyopata ajali ilikuwa katikati.

Taarifa kutoka eneo la tukio na chanzo cha ajali

Bado hakuna uhakika wa taarifa rasmi kuhusu chanzo cha ajali hiyo lakini taarifa zilizopo zinadai kuwa ni kutokana na mfumo wa breki za gari hilo kushindwa kufanya kazi na hivyo dereva kushindwa kumudu usukani na gari kutumbukia korongoni.

Aidha taarifa nyingine zinadai kuwa dereva huyo alikuwa katika mwendo kasi eneo hilo ambalo lina mteremko mkali na kona kali  hivyo kushindwa kuhimili mwendo kasi wa gari lake.

Lakini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo aliwaambia waandishi wa habari kwamba polisi bado wanachungunza chanzo cha ajali hiyo na taarifa itatolewa kwa umma uchunguzi huo utakapokamilika.

Taarifa zilizopatika kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa wanafunzi 29 walifariki papo hapo pamoja na walimu wao wawili na dereva wa gari hilo na kufanya idadi ya waliokufa wakati huo kuwa 32.

Majeruhi walikimbizwa katika hospitali teule ya Wilaya Karatu na kituo cha afya cha Rhotia  ambapo inaelezwa kuwa watatu walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali teule na majeruhi watatu walihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ambapo mmoja alifariki dunia saa 10 jioni hivyo kubakia wawili ambao wote ni wasichana.

Habari kutoka kwa mashuhuda wa ajali zinadai kuwa polisi wakishirikiana na wananchi wa kijiji hicho pamoja na wapita njia walianza uokoaji mara moja baada ya kutokea kwa ajali.

Kutokana na kuharibika vibaya kwa gari hilo wananchi  hao walitumia mashoka, mitarimbo, nyundo, majembe na vifaa vingine kutoa miili ya marehemu na majeruhi.

“Hali ilikuwa ya kutisha na kuogofya katika eneo la ajali, miili mingi iliyotolewa ilikuwa na majeraha makubwa ya kutisha na wengi walikuwa wamevunjika viungo vyao,” alidai mmoja kati ya waokoaji ambaye hakutaka kutajwa gazetini.

Majonzi, vilio, Mount Meru Hospitali

Hali ilikuwa ya kusikitisha katika Hospitali ya Mount Meru ambapo vilio, majonzi, simanzi vilitanda kila kona na kila mmoja  wakiwamo madaktari, wauguzi, viongozi wa serikali na wa kisiasa walionekana kuguswa na tukio hilo.

Umati mkubwa wa wakazi wa Arusha na vitongoji vyake  ulianza kukusanyika kuanzia saa 6 mchana baada ya taarifa kuzagaa kuwa majeruhi pamoja na miili ya waliofariki ilikuwa njia kuletwa hospitalini hapo.

Hadi kufikia saa 9 alasiri eneo lote la hospitali lilikuwa limefurika watu na barabara maarufu ya Afrika Mashariki nayo ilikuwa imefurika kiasi kwamba magari yalilazimika kupita kwa taabu.

Aidha eneo la kuhifadhia chumba cha maiti nalo lilikuwa limefurika watu ambao walikuwa wakisubiri kuona na kutambua miili ya wapendwa wao hali iliyowalazimu polisi wa kikosi cha FFU waliokuwa na silaha nzito kuimarisha ulinzi.

Ilipotimu saa 9.46 alasiri miili ya majeruhi watatu iliwasili kwa magari ya kubeba wagonjwa (ambulance) na ndipo viliposikika vilio kutoka kila kona ya viwanja vya hospitali hiyo.

Baadaye umati huo ulihamia katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti na miili ilipowasili polisi walishindwa kuthibiti hali kutokana na wazazi na ndugu wa marehemu kushinikiza kuwa wanataka kutambua miili ya watoto wao.

Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Mkuu wa Wilaya Arusha, Gabriel Dagharo, kuingilia kati na kuwataka wale tu waliofiwa waruhusiwe kuingia ndani ya chumba cha maiti kutambua miili ya watoto wao.

Kauli za viongozi

Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Dagharro, alisema binafsi na serikali amesikitishwa na msiba huo na kuongeza kuwa, serikali iko pamoja na wazazi walipoteza watoto wao.

“Msiba huu umetugusa wote, si msiba wa watu wa Arusha peke yao huu ni msiba wa taifa na ndiyo maana Rais wetu ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na watu wote wa Arusha,” alisema.

Alisema wakati viongozi wa serikali wakikutana kufanya taratibu za mazishi kwa kusaidiana na familia ibada ya pamoja ya kuaga miili itafanyika katika uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid siku ya Jumatatu kuanzia saa 6 za mchana.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema anaungana na wazazi na wanafamilia katika kipindi hiki kigumu cha kupotea kwa maisha ya wanafunzi hao na walimu wao.

“Hakuna jambo limetuumiza watu wa Arusha kama ajali hii, natoa pole kwa wazazi na wamiliki wa shule. Naomba tuungane sote bila kujali itikadi zetu za kisiasa na imani zetu za dini huu msiba ni wetu sote watu wa Arusha na Watanzania kwa ujumla,” alisema.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Longino Vicent Nkana, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanafunzi hao waliondoka shuleni hapo saa 12.30 asubuhi  kuelekea Karatu kwa ajili ya kushiriki mitihani hiyo ya ujirani mwema.

Alieleza kuwa wamekuwa wakifanya mitihani hiyo ya ujirani mwema kwa wanafunzi wa darasa la saba kwa zaidi ya miaka mitatu sasa na hakukuwahi kutokea tatizo lolote.

“Magari yetu hufanyiwa matengenezo katika karakana zetu mbili kila wiki na yako salama na hata wakati mwingine tunakodishwa kwa shughuli nyingine za kijamii,” alifafanua.

Aliongeza kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 2006 na imekuwa katika shule bora kitaaluma mkoani Arusha ambapo mwaka 2016 ilishika nafasi ya pili ngazi ya mkoa katika mitihani ya darasa la saba.

Majina ya waliofariki

Majina ya waliofariki yaliyopatikana ni pamoja na Mteage Amos, Justine Alex, Irene Kishari, Gladness Goodluck, Praise Roland, Shadrack Biketh, Junior Mwashuye, Aisha Said, Oumligh Herri Rashid, Gema Gerald, Rebecca Daudi, Hagai Lucas, Said Ally na Ruth Ndemna.

Wengine ni Atusa Kassim, Neema Eliwashi, Neema Martine, Greyson Robson Masana, Heavennight  Enock, Ian Tarimo Anold Alex, Naomia Hosea, Rukia Altam, Eliapendo Elihudi, Marion Mrema, Rehema Msuya, Sabrina Said na Prisca Charles.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad