Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani hapa limesitisha huduma za umeme katika mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira (Kiwira Coal mine) na ofisi za Jeshi la Polisi mkoani hapa baada ya taasisi hizo kushindwa kulipa madeni zinazodaiwa na shirika hilo.
Meneja wa Tanesco Mkoa Mbeya, Benedict Bahati amesema mgodi wa Kiwira unadaiwa Sh1.3 bilioni na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linadaiwa Sh700 milioni.
Bahati amesema wamefikia hatua hiyo kwa sababu wadaiwa hao hawajaonyesha nia ya kulipa madeni yao ambayo ni ya muda mrefu na hivyo kulisababishia shirika hilo kushindwa kujiendesha kwa ufanisi.
“Taasisi za Serikali ambazo madeni yake ni makubwa na mwitikio wake wa ulipaji sio mzuri, tumesitisha huduma mpaka watakapolipa madeni hayo,”amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari amekiri kudaiwa deni na Tanesco pamoja na kusitishiwa huduma hiyo kwenye baadhi ya vitengo na kwamba wao kama taasisi wanadaiwa kama ilivyo kwa taasisi nyingine.