Wakati watu wasiojulikana wakiendelea kuua viongozi wa vijiji licha ya Jeshi la Polisi kuweka kambi, aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Mashishanga ameitaka Serikali ijitathmini akisema matukio hayo ya mkoani Pwani yanaitia doa.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha mauaji hayo yanakomeshwa mara moja ili shughuli za uzalishaji mali ziendelee kama kawaida, badala ya wananchi kuishi kwa hofu ya kutofahamu nani atafuata katika orodha ya wanaosakwa kuuawa.
Watu 31 wameshauawa katika kipindi cha kuanzia Mei mwaka jana na mauaji ya viongozi wa vijiji yamekuwa yakishabihiana, huku askari wa Jeshi la Polisi wakiuawa katika mashambulizi.
Viongozi 15 wa serikali za vijiji na vitongoji vya wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti, polisi kumi, watumishi wawili wa Idara ya Maliasili, mwanachama mmoja wa CCM na watu watatu waliokuwa wamevaa nguo za kike wameshauawa katika kipindi hicho.
Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijaeleza kama wanaofanya mauaji hayo katika vijiji hivyo, ambavyo baadhi vinapakana na hifadhi za taifa, ni majambazi, magaidi au majangili.
“Hatupendi kuona haya yanayotokea yakitendekea na kuendelea kusikika kila siku kana kwamba hatuna vyombo imara vya ulinzi na usalama,” alisema Mashishanga alipozungumza na gazeti hili katika Mkutano Mkuu wa 22 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB unaomalizika leo jijini Arusha.
Jeshi la Polisi limeweka kambi katika Kijiji cha Jaribu katika jitihada za kukabiliana na mauaji hayo na Wizara ya Mambo ya Ndani imetangaza katika bajeti yake ya mwaka 2017/18 kuwa itaunda mkoa maalumu wa kipolisi utakaojumuisha wilaya hizo tatu, lakini watu hao wameshaua makada wawili wa CCM na kujeruhi watu wawili tangu Waziri Mwigulu Nchemba atangaze uamuzi huo.
Katika tukio la wiki hii, watu wasiojulikana walimuua kwa risasi mwenyekiti wa CCM wa Tawi la NjiaNne, Iddy Kirungi aliyekuwa akijaribu kukimbia baada ya kuwaona wauaji waliokuwa wamemjeruhi mtoto wake.
Mtoto huyo alikuwa akielekea bafuni na inaonekana wauaji walidhani kuwa ni mwenyekiti huyo na kumrushia risasi. Siku tano kabla ya tukio hilo, watu hao walimuua kwa risasi aliyekuwa katibu wa CCM wa Kata ya Bungu, Alife Mtulia wakati akielekea bafuni kuoga.
“Ni aibu kwa kinachoendelea. Serikali iangalie imekosea wapi au wananchi wake wamefanya nini hadi hali hiyo ikatokea na ikomeshe matukio hayo,” alisema Mashishanga, ambaye kwa nafasi ya ukuu wa mkoa alikuwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama.
Kwa uzoefu wake, alisema huenda dhuluma ikawa chanzo hivyo uchunguzi ufanywe haraka na kurekebisha kasoro zitakazobainika ili wananchi wa mkoani humo waishi kama ilivyo maeneo mengine.
“Wakati mwingine viongozi wanajisahau katika maamuzi yao. Bila kujua wanaweza wakawa wanapandikiza chuki na kusababisha kisasi ambacho kinaweza kuhusisha vifo vya namna hii,” Mashishanga alieleza shaka yake.
Maeneo yenye shaka, alisema mkuu huyo wa zamani, ni masuala ya uhusiano hasa wa ndoa, mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya vyama kwa ngazi za wilaya au uporaji mali kwa kutumia mamlaka ndiyo yanaweza kusababisha mauaji hayo.
Mashishanga pia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kurudisha imani ya wananchi katika masuala mbalimbali.
“Ni kazi ngumu kuondoa wasiwasi na shaka ya wananchi kwa muda mfupi, lakini Serikali ya awamu hii imeweza. Hata mwananchi wa kawaida ana uhakika wa kufanikisha akitakacho bila kusumbuliwa kama ilivyokuwa awali,” alisema kiongozi huyo aliyehudumu kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne.
Mashishanga pia alizungumzia kuacha kazi kwa aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki akisema kumetokana na tathmini binafsi iliyofanywa na kiongozi huyo na kuona hawezi kuendana na kasi iliyopo.
Credit - Mwanachi