Askofu Mokiwa Aamua Kuanzisha Kanisa lake Nyumbani Kwake


ALIYEKUWA Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam,  Valentino Mokiwa anadaiwa kufungua  kanisa nyumbani kwake. 

Gazeti hili juzi lilielezwa kuwa  licha ya   Dk. Mokiwa kuvuliwa uaskofu na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya, bado anaendelea kutoa huduma ya kiroho kama kawaida. 

“Kanisa hilo lipo nyumbani kwake Mtaa wa Kilimani, Mbezi kwa Yusuph… watu wanaendelea kusali kama kawaida,” kilisema chanzo chetu (jina tunalihifadhi). 

Jana, MTANZANIA lilifika eneo hilo na kushuhudia baadhi ya waumini wakiondoka kwenda majumbani kwao baada ya ibada kumalizika. 

Waumini hao  hawakuwa tayari kuzungumza lolote na mwandishi wa gazeti hili wakidai kuwa si wasemaji. 

Juhudi za kuonana na Dk. Mokiwa hazikufanikiwa kwa sababu mwandishi  alizuiwa na walinzi. 

Mahojiano  ya mlinzi na mwandishi  yalikuwa kama ifuatavyo: 

Mlinzi: Ni kweli hapa ni nyumbani kwa Askofu Mokiwa, wewe ni muumini? 

Mwandishi: Ndiyo. 

Mlinzi: Unaishi wapi? 

Mwandishi: Naishi Mbezi Mwisho, nilikuwa na kawaida ya kwenda kusali kule Posta, nimesikia baba yupo hapa  ndiyo nikaja. 

Mlinzi: Pole, ibada imeshamalizika,  njoo Jumapili ijayo mapema. 

Mwandishi: Hakuna ibada  katikati ya wiki? 

Mlinzi: Hakuna, njoo Jumapili. Ibada huwa inaanza saa nne kamili asubuhi. 

Wakati mahojiano hayo yakiendelea, mwandishi alishuhudia viti vingi ambavyo vilikuwa vimepangwa  eneo hilo chini ya hema. 

Kwa kuwa hakufanikiwa kuonana na Dk. Mokiwa, mwandishi alilazimika kuwasiliana naye kwa simu lakini hakuwa tayari kueleza kwa kina kuhusu suala hilo. 

Mahojiano yalivyokuwa: 

Mwandishi: Bwana Asifiwe Baba Askofu 

Dk. Mokiwa: Amen 

Mwandishi: Baba Askofu nilifika   hapo nyumbani kwako  sikuruhusiwa kuingia ndani. Kuna taarifa kwamba umefungua kanisa nyumbani kwako, je ni kweli? 

Dk. Mokiwa: Aliyekuambia nimefungua kanisa ni nani? 

Mwandishi: Nimejulishwa na chifu (Mkuu wangu wa kazi) ofisini. 

Dk. Mokiwa: Yeye alijulishwa na nani, huyo chifu wako ana namba za huyo aliyempigia… basi ampigie, amuulize, amwambie zaidi juu ya jambo hilo na mimi nipate jina la huyo mtu na namba zake kwa sababu nataka kuzijua. 

Mwandishi: Lakini Baba Askofu, kimaadili haturuhusiwi kumuandika mtu aliyetupatia taarifa. 

 Dk. Mokiwa: Sasa taarifa za uhakika unazitaka kutoka kwangu mimi au kwa aliyeleta taarifa kwenu. 

  Mwandishi: Tunahitaji uthibitisho kutoka kwako. 

Dk. Mokiwa: Uthibitisho wa nini? Aliyewaletea ndiyo athibitishe, huwezi kuulizwa swali na mtu mwingine halafu unakuja kupata uthibitisho kwangu, hiyo inakwenda sawasawa? 

Mwandishi: Asante Baba Askofu 

Kauli ya kanisa 

MTANZANIA liliwatafuta viongozi wa juu wa kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam  kupata kauli yao juu ya suala hilo. 

Mmoja wa viongozi hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini   alisema hana taarifa rasmi kuhusu suala hilo. 

“Binafsi sina taarifa hizo, ndiyo kwanza nazisikia kwako… siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu hatuna taarifa rasmi,” alisema. 

MTANZANIA lilitaka kujua iwapo itathibitika kweli ameanzisha kanisa, kanuni, sheria na taratibu za kanisa hilo zinaelekeza vipi na watachukua hatua gani? 

Alisema kwa sasa ni vigumu kufafanua hilo kwa sababu haijajulikana kama kweli Dk Mokiwa ameanzisha kanisa au la. 

“Kwa kuwa hatuna taarifa rasmi, hatuwezi kusema kanuni zinasemaje, hatujui kama kweli kaanzisha kanisa au ni kikundi cha maombi tu kinakutana nyumbani kwake. 

“Kuna tofauti ya kanisa na kikundi cha maombi. Tunahitaji kufanya utafiti tupate habari rasmi ndiyo tuweze kusema kaanzisha kanisa au la. 

“Kanisa lazima liwe na usajili na jina, kwa sasa ni  mapema mno kusema kaanzisha kanisa au la,” alisema. 

Dk. Mokiwa, alivuliwa uaskofu Januari, mwaka huu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa maadili ya kanisa na kukiuka miiiko ya kanisa. 

Uamuzi huo uliibua mvutano mkubwa ndani ya kanisa hilo na kuzaa makundi mawili hasimu ambako moja linamuunga mkono Dk. Mokiwa na jingine limebaki likimuunga mkono Dk. Chimeledya. 

Hali hiyo ilisababisha mtikisiko mkubwa uliotishia kupasuka kwa kanisa hilo. 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad