Mkazi wa Kitangili, Shinyanga Francis Kilalo (31)anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora kukutwa na sare na vifaa vingine vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) ambavyo anatuhumiwa kuvitumia kupateli na kuwadanganya wananchi kwa kuchukua fedha kutoka kwa vijana wanaotafuta nafasi ya kujiunga na Jeshi hilo.
Taarifa hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Mkoa wa Tabora Wilbroad Mtafungwa alipozungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake juu ya hatua mbalimbali walizochukua katika kupambana na uhalifu mkoani humo.
Amesema kuwa polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo katika Hoteli ya JM iliyopo Wilayani Igunga akiwa na sare mbalimbali za JWTZ zikiwa na cheo cha Koplo ambavyo ni pamoja na kofia tatu, begi, sweta, buti jozi moja, magwanda na mikanda mitatu.
Mali nyingine zilizokamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni pamoja na fomu za likizo cha likizo , fomu za kujaza vijana wanaotaka kujiunga na Jeshi hilo na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) kwa mujibu wa Sheria na hiari na mihuli zenye nembo inayofanana na Jeshi hilo.
Kamanda Mtafungwa alisema kuwa mtuhumiwa alikuwa akitumia nyaraka na sare za Jeshi hilo kuchukua fedha kwa kuwadanganya na kuwatapeli wananchi mbalimbali kwa kudai atawatafutia ajira katika majeshi ya Kujenga Taifa na la Wananchi.
Kamanda huyo wa Mkoa wa Tabora aliongeza kuwa mtuhimiwa huyo pia alikutwa barua kutoka Serikali za mitaa za Dar es Salaam na gari aina ya Toyota Starlet yenye namba za Usajili T633 ARF ambalo wanaendelea kuchunguza uhalali wa umiliki wake.
“Pia tumebaini kuwa gari hilo hilo, mtuhumiwa alikuwa akilitumia na kuwafanya baadhi ya wananchi wamuamini kuwa atawasaidia kupata nafasi katika majeshi,” amesema Kamanda
Ameongeza kuwa mtuhimiwa huyo pia alikuwa na barua za maombi ya watu ya kuomba kujiunga na Jeshi, Fomu za Matibabu za Hospitali ya Jeshi ya Lugalo na nakala ya Vyeti vya kumaliza elimu ya Sekondari vya baadhi ya watu.
Kufuatia tukio hilo alitoa wito kwa waananchi waliowahi kutapeli ndani na nje ya Mkoa wa Tabora kujitokeza katika vituo vya Polisi ili waweze kutoa ushahidi utakasaidia kuonyesha ni jinsi gani walivyumizwa na mtuhumiwa huyo.
Kamanda Mutafungwa alisema kuwa Polisi inaendelea kushirikiana na JWTZ ili iweze kubaini sare na vifaa hivyo alivipata wapi , kwa lengo lipi na ni nani aliyompatia ili wahusika wote waweze kufikishwa katika vyombo vya Sheria kwa hatua zaidi.