Simba italazimika kukaza msuli ili kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani baada ya Mbao FC kuitoa Yanga kwa kuifunga bao 1-0 katika mchezo mkali wa nusu fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Ushindi wa Mbao, umeivua Yanga ubingwa wa mashindano hayo na sasa kombe linabakia kumpata bingwa mpya iwe Mbao ama Simba katika mechi ya fainali itakayopigwa mwishoni mwa mwezi huu baada ya kumalizika kwa mechi za Ligi Kuu. Simba iliingia fainali baada ya kuitoa Azam kwa bao 1-0.
Ushindi wa Mbao ni kama umevuruga mipango ya Simba na kuamsha upya presha yao ya kusaka tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.
Hali hiyo iko vipi, Simba ilikuwa ikitarajia mteremko wa Yanga ambayo ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, kwani hata kama ingeifunga katika fainali ya FA na huku imetwaa ubingwa wa Bara, ni wazi Simba ingepanda ndege kuwakilisha Kombe la Shirikisho.
Simba sasa wanatakiwa kutumia nguvu zao wenyewe kusaka tiketi hiyo mwakani kwa kuhakikisha wanaifunga Mbao FC kwenye mchezo wa fainali.
Ikiwa hali haitakuwa hivyo, salama ya Simba ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuacha Mbao ambayo ishinde ama ifungwe na Simba, itacheza Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, Simba inaweza vilevile kukosa yote kwani, pamoja na kujipa matumaini makubwa, inaweza isitwae ubingwa wa Ligi Kuu na pia ikapoteza mchezo wake wa fainali na Mbao na kuwaacha wauza mbao hao wakiweka rekodi ya kuingia Ligi Kuu na moja kwa moja kuiwakilisha Tanzania kimataifa.
co cha uchungu,cha nguruwe na refa wo
ReplyDelete