Uongozi wa kampuni ya Acacia, inayomiliki mgodi wa Buzwagi, jana ulitoa taarifa ya kupunguza wafanyakazi zaidi ya 100 wakati ikijiandaa kufunga mgodi huo ifikapo mwaka 2020.
Meneja mahusiano wa kampuni hiyo, Nector Foya alisema kuwa taarifa ya kupunguza wafanyakazi ilitolewa baada ya meneja mkuu wa Buzwagi, Stewart Hamilton kuzungumza na wafanyakazi wa mgodi huo jana.
“Ni kweli taarifa hiyo imekuja baada mkurugenzi kuzungumza na wafanyakazi wa mgodi leo (jana),” alisema Foya.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa wafanyakazi 100 watapunguzwa baada ya kufanyika vikao mbalimbali katika wiki mbili, kuanzia jana ikiwa ni pamoja na kujibu maswali mbalimbali.
Mbali na upunguzwaji huo, taarifa inaeleza kuwa wafanyakazi hao watatoka katika idara zinazotoa msaada na huduma.
“Tutaanza mawasiliano na jamii zetu na kulenga matumizi yetu katika mradi endelevu ya jamii inayoweza kuchangia katika kuifanya jamii iweze kujitegemea baada ya 2020,” inaeleza taarifa hiyo.
Aidha taarifa inaeleza kuwa uchimbaji wa mgodi huo utaanza kumalizikia katika robo ya nne ya mwaka na uchimbaji utaishia mwisho wa Desemba 2017 na uchenjuaji utaisha 2020.