Mshambuliaji nyota wa Yanga, Donald Ngoma ambaye sasa ni majeruhi amesema kuwa hana mpango wa kujiunga na klabu ya Simba mara mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa mwezi ujao.
Ngoma alisema hayo baada ya kuwepo uvumi jijini Dar es Salaam na kwenye mitandao kuwa kutoonekana katika kikosi cha timu hiyo kumetokana na mkakati wake wa kujiunga na wapinzani wa jadi wa klabu yake ya sasa.
Alisema kuwa kuwapo kwake nje kumetokana na kuumia na si vinginevyo na wala hana mgomo wa kuichezea timu hiyo kama inavyosambazwa na watu mbalimbali.
“Yapo mengi yamesemwa kuhusu mimi, mengi siyo kweli, kazi yangu ni mpira na mchezaji yeyote huwa anapenda kucheza na wala si kukaa benchi.
“Naomba nisihusishwe na Simba au timu yoyote, bado ni mchezaji halali wa Yanga, naheshimu mkataba,” alisema Ngoma.
Alifafanua kuwa uongozi wa klabu hiyo (Yanga) umempa ruhusa ya kupumzika na wala hajatoroka kwenda Afrika Kusini kutafuta timu zaidi ya kufuata matibabu ya kisasa.
Mchezaji huyo kutoka Zimbabwe alisema kuwa hadi sasa hajasaini mkataba mpya na klabu hiyo pamoja na kuwa tayari kufanya hivyo endapo watakubaliana na masharti yake.
“Siwezi kusema kama nitaondoka au la, itategemea uamuzi ya wakati huo na hasa ule wa uongozi, kwa sasa nimepata nafuu na nitaanza mazoezi karibuni,” alisema.