BUNGE limeishauri serikali kutoa kibali cha ajira mpya za madkatari na wataalamu 519 na fedha katika Hospitali ya Mafunzo Mlongazila jijini Dar es Salaam ili ianze kutoa huduma.
Ushauri huo ulitolewa bungeni mjini hapa juzi na Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa mwaka ujao wa fedha.
Mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe, akiwasilisha taarifa ya kamati, alisema walitembelea mradi Machi 21 na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa hospitali, lakini kuna changamoto ya upatikaji wa fedha kutoka serikalini na upungufu wa watumishi.
Alisema wakati wanatembelea mradi huo, ulikuwa umekamilika kwa kiasi kikubwa ikiwamo kuwapo kwa vifaa vya kisasa.
Alisema mradi huu ni moja kati ya miradi mikubwa nchini ukiwa na gharama ya Dola za Marekani 94,540,000 (Sh. bilioni 210.6) ambazo ni mkopo wa riba nafuu wa Dola 76,500,000 na mchango wa serikali ya Tanzania wa Dola 18,040,000.
"Katika mwaka huu wa fedha, chuo kiliomba jumla ya Sh. bilioni 14.549 kwa utaratibu maalum (special arrangement) kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vitendanishi na matumizi mengine," Bashe alisema.
"Wakati kamati inatembelea mradi, hakuna fedha iliyokuwa imetolewa. Hata hivyo, waziri aliiahidi kamati kuwa, kufikia Aprili mwaka huu, itakuwa imetoa kiasi cha Sh. bilioni tano kwa ajili ya kuanza kununua vifaa tiba."
Aliongeza kuwa, pamoja na changamoto ya fedha, bado chuo kina upungufu wa rasilimali watu kwa kuwa mahitaji ni watumishi 900 na mpaka kamati inatembelea, waliopatikana ni watumishi 381, sawa na asilimia 42.3 ya mahitaji yote.
"Kamati inatoa rai kwa serikali kuhakikisha watumishi wote 900 wanapatikana ili kuweza kutoa huduma kwa wagonjwa, kinyume cha hapo ni kutoutendea haki mradi huu mkubwa na mzuri wenye vigezo vya hospitali za kimataifa," alisema.
Mbunge huyo wa Nzega Mjini (CCM) pia alisema kamati yao inaona uwekezaji huo mkubwa ni vyema uende sambamba na utolewaji wa fedha za kutosha ili utoe matunda tarajali.