Ben Pol Huo ni Ushamba na Umejidhalilisha! Wabongo si Watu wa Utupu

 


BENARD Paul ndilo jina lake halisi, lakini mashabiki wanamfahamu zaidi kama Ben Pol, yule kijana mweusi, mrefu ambaye nyuma ya kipaza sauti, anafanya vizuri katika Muziki wa Kizazi Kipya, akiwa amejizatiti zaidi katika R&B. Ana sauti nzuri na kwa kweli anaimba vizuri, licha ya baadhi ya nyakati kudaiwa kuwa anakopi na kupesti nyimbo za nje, kitu ambacho naye amekuwa akikanusha mara kadhaa.

Ana nyimbo nyingi, lakini katika ushirika wake na rapa Darassa, ameunogesha kwa kiwango cha kutosha ule Wimbo wa Muziki.

Hawezi kuwa top katika aina hiyo ya muziki, lakini huwezi pia kumshusha kivile, maana anajua nini anafanya. Nikiri, sijawahi kukutana na huyu dogo, lakini ni mfuatiliaji mzuri wa kazi zake na mara kadhaa, nimewahi kuongea naye kuhusu masuala mbalimbali ya kikazi.



Anazungumza vizuri, kitu kinachonifanya nimtabirie kama muungwana. Juzikati nilimsikia Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Godfrey Mngereza akilaani picha za utupu za msanii huyo alizotupia katika akaunti yake Instagram na kusababisha kizaazaa kwa mashabiki, wengi wakimponda na wachache wakimtetea. Mngereza aliwataka wasanii kufanya kazi nzuri ambazo zinaweza kuwaweka sehemu nzuri na siyo kutengeneza mazingira ambayo yanautia dosari muziki wao. Alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa kuzingatia utamaduni wetu, licha ya kusema kabla ya kuchukua hatua, watamuita na kumsikiliza.

Lakini pengine kwa kuzidiwa  na mashambulizi, kijana huyo mwimbaji wa Kibao cha Phone, alijitokeza tena na kutoa ‘clip’ ya video ikimuonyesha akiwa mtupu huku akiimba na kusindikiza na maneno ya kuwaambia watu kuwa wasijaribu kutoa hukumu kwa kitabu ambacho bado hawajasoma.



Ujumbe wake kwa mashabiki ni kuwa walipaswa kujua nini maana ya yeye kuweka picha ile, kwani alikuwa anawawekatayari mashabiki zake kwa ujio wake mpya wa video ya wimbo uitwao Tatu.

Baada ya ufafanuzi huo, kuna baadhi wamekubaliana naye na wengine wameendelea kumponda. Mimi sikubaliani naye na wala simpondi, isipokuwa ninachotaka ni kumpa somo kama mdogo wangu, kama shabiki wa muziki wake mzuri na pia kama mdau. Ben Pol kwa nafasi yake, ni kama balozi wa ndani mwenye wajibu wa kuhakikisha taifa halipotoki kimaadili, hasa vijana wanapohusika.

Ninajua wasanii hivi sasa wako katika vita kubwa ya kujaribu kuwa na ubunifu ili kuweza kutangaza kazi zao zipate kukubalika kitaifa na kimataifa, lakini ni makosa makubwa kufanya ubunifu unaopingana na utamaduni wako.

Wabongo si watu wa uchiuchi, ndiyo maana kila siku tunawapigia kelele wadada wa Bongo Muvi, tunawaambia kuwa kwao nusu utupu hakuwafanyi wauze kazi zao, zaidi kunawadhalilisha, kwani mashabiki wanataka simulizi nzuri, zenye mafunzo kwao na zinazowakilisha utamaduni halisi wa Mtanzania. Hata kama nia yake ilikuwa nzuri kiasi gani, ni jambo la fedheha kijana wa kiume kupiga picha za video ukiwa mtupu.

Ili iweje sasa? Haya tuseme huo wimbo wake wa Tatu, hivi ni kweli mawazo yake yote yaliishia kwenye utupu? Hapana, huu ni ufinyu wa utambuzi wa mambo. Tatizo moja la msingi kwa vijana wetu ni kule kutaka kwao kuleta Umarekani katika kila jambo. Walianza kusuka nywele, wakaja kutoboa pua, wakavalia suruali zao katikati ya makalio na sasa wanataka kuwa uchi kabisa. Tuache ushamba huu, hasa nyinyi ambao mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutuongoza. Kama tutatukuza utamaduni wa watu, ni lini watu wataufahamu wa kwetu? Au ulitaka kuwaonyesha watu jinsi ulivyobarikiwa umbo zuri lenye mvuto? Hakika umejidhalilisha!

NA OJUKU ABRAHAM,
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad