Taarifa iliyotolewa na BoT inawataka wenye amana, wadai na wadaiwa kuwa wavumilivu wakati mfilisi akiandaa utaratibu wa kushughulikia stahiki zao.
“Mfilisi kwa wakati muafaka atawafahamisha wenye amana, wadai na wadaiwa utaratibu wa malipo ya madai, ulipaji wa madeni na taratibu nyingine zinazohitajika kwa mujibu wa sheria,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Uamuzi huu wa BoT umetolewa baada ya hukumu ya kesi ya utakatishaji fedha iliyokuwa ikiikabili benki hiyo kutolewa.
Itakumbukwa, mwaka 2014, Mtandao wa Kudhibiti Uhalifu wa Masuala ya Fedha (FinCEN) wa Marekani uliitaja FBME kuwa taasisi inayojihusisha na utakatishaji fedha hivyo kuizuia kutoa huduma nchini humo.
Machi mwaka jana, msimamo wa FinCEN uliendelea kuwa huohuo hata Aprili 14, mahakama moja jijini Washington, DC ilitoa hukumu inayoupendelea mtandao huo. Nakala za hukumu hiyo imetumwa kwa BoT na Benki Kuu ya Cuprus kwa hatua zaidi.
Baada ya hukumu hiyo iliyosomwa na Jaji Christopher Cooper, benki hiyo yenye makao makuu yake nchini na matawi huko Cyprus italazimika kurudisha Dola 2.6 bilioni za Marekani ambazo ni amana za wateja wake ndani ya siku 90.