Aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema mapendekezo yanayotolewa na CAG katika ripoti yake ya ukaguzi hayatekelezwi kikamilifu na watendaji wa serikali, jambo linalosababisha makosa hayo kujirudia na kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma.
Utouh ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uwajibikaji wa Umma ya Wajibu (WIPA), amesema kwa mamlaka za serikali za mitaa pekee, CAG alitoa mapendekezo 79, kati ya hayo ni matatu tu sawa na asilimia 4 ndiyo yalitekelezwa wakati asilimia 44 yalikuwa kwenye utekelezaji na asilimia 52 hayakutekelezwa kabisa.
Utouh amesema watendaji wa Serikali wamekuwa wakipuuzia mapendekezo hayo kwa sababu hawawajibishwi kwa makosa yao.
Mkurugenzi huyo amesema hata miongozo inayotolewa na Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC) haitekelezwi hata pale kunapobainika makosa ya wazi.
"Mwaka wa fedha uliopita, kamati ya LAAC ilitoa miongozo 1,094 kwa mamlaka za serikali za mitaa, miongozo 438 sawa na asilimia 40 yalitekelezwa, 230 sawa na asilimia 21 yalikuwa katika hatua za utekelezaji na 427 sawa na asilimia 39 hayakutekelezwa kabisa," amesema Profesa Utouh