Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewapongeza wabunge wake wateule wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).
Wabunge waliochaguliwa na Bunge la Tanzania kutoka kundi C ni Josephine Lamoyan na Pamela Maassay.
Chadema imesema ina imani kubwa kuwa wabunge hao wateule wa Eala watakuwa wawakilishi bora wa nchi kwenye Bunge hilo wakizingatia manufaa, masilahi na matakwa ya Watanzania na wananchi wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Taarifa ya pongezi ya Chadema inasema kupitia uwezo, uzoefu na u-tayari walionao wa kujifunza na kupokea maarifa mapya; Lemoyan na Maassay watabeba matumaini ya mabadiliko ya Watanzania, ambao wangependa kuona ushirikiano wa EAC unakuwa na nguvu za kiuchumi na kisiasa uliojengwa katika misingi ya kidemokrasia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi.
“Chama kinawaahidi ushirikiano wakati wowote watakapohitaji ili waweze kutimiza wajibu na majukumu hayo kwenye uwakilishi wa Eala na EAC kwa jumla kwa niaba ya nchi yetu,” imesema taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema Tumaini Makene baada ya uchaguzi uliofanyika jana (Jumatano).