Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kati ya mwaka 1993 hadi 2005, Andrew Chenge, jana alifunguka kuhusu sakata la usafirishaji wa mchanga wa dhahabu kwenda nje ya nchi.
Hata hivyo, akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Chenge alisema ripoti ya Jaji Mark Bomani ilikuwa ndio mwarobaini wa usafirishaji mchanga huo nje kama mapendekezo yake yangefanyiwa kazi.
“Yawezekana nyinyi hamkumbuki historia. Ripoti ya Jaji Bomani ilitoa mapendekezo ya Serikali ione uwezekano wa kufanya smelting (kuchakata) hapa nchini,” alisema.
“Mtu akikumbumsha kwa jambo jema (kama Rais John Magufuli alivyofanya), atakuambia kwanini hamjafanya toka wakati huo, labda kuna sababu. Lipo kwenye ripoti ya Jaji Bomani.”
“Ukisema kwamba requirement (mahitaji) ya smelter (mtambo) kwa maana ya gharama na production (uzalishaji) iliyopo itakuwa gharama sana basi waambie Watanzania.”
“Unatakiwa ujibu hiyo kwamba production iliyopo pale Buzwagi na Bulyanhulu haitoshelezi na useme je ni suala la umeme au nini au ni hayo makenikia uwaeleze Watanzania watakuelewa.”
Alipoombwa maoni yake kwamba akiwa AG ndipo mikataba mingi iliingiwa, Chenge alikuwa mkali, akihoji “AG kwa kitu gani. AG kwa kitu gani? Rais ameshatoa maoni yake, kuna marais wawili?”
Alisema akiwa Serikalini na Rais wa awamu wa kwanza, Jullius Nyerere walianza na kufafanua kuwa yeye ni mtanzania aliyesomeshwa na kubobea katika mikataba ya madini na petroli.
“Nasema Rais (Magufuli) ameamua kuwakumbusha mapendekezo ya Bomani ambayo kama tungeyatekeleza tusingefika hapo. Baaada ya hapo sasa ndio muulizane inawezekana au haiwezekani?”