DARASSA, Mbona Umekopi na Kupesti..!!!!?


NIANZE kwa kutoa pole kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa familia za wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent, ya jijini Arusha, ambao wamepoteza maisha yao katika ajali mbaya kabisa ya gari, iliyoua watu 36.

Huu ni msiba wa taifa zima na kwa kweli wiki hii bendera zilipaswa kupepea nusu mlingoti.

Baada ya pole hizo, sasa nirejee kwenye mada yangu ya leo, ambayo ni barua yangu kwa msanii mkubwa wa Hip Hop nchini, Shariff Thabeet, ambaye wengi tunamtambua vizuri zaidi kwa jina la Darassa.

Ingawa alianza kufanya muziki siku nyingi, lakini wengi wamekuja kutambua uwezo wake baada ya kutoa kibao ambacho kiligeuka kuwa wimbo wa taifa, Muziki.

Wimbo uliomfanya hata nchi za jirani kumpa shoo, huku Watanzania walioko ng’ambo wakiufaidi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Darassa wewe ni mkali, ila ufundi wako wa kwenye Wimbo wa Muziki ulikufanya utambulike vyema. Nimeusikiliza na kuangalia video ya kazi yako mpya, Hasara Roho, dah!

Video ni nzuri lakini mtazamo wa mashabiki wengi ni kuhusu kukopi na kupesti mtindo uleule ulioimba kwenye Muziki. Umewaangusha sana kaka.

Swali langu kwako, Darassa umekosa ubunifu, umekosa usimamizi, washauri wazuri wa biashara ya muziki au ni haraka zako za kutaka kuachia ngoma mpya?

Kila shabiki alikuwa anasubiri ujio wako mpya, kwa sababu wengi waliamini Muziki ulibahatisha, isipokuwa wachache, nikiwemo mimi, ambaye nautambua uwezo wako tangu zamani.

Wimbo huu mpya kwa kweli umekur-udisha nyuma badala ya kwenda mbele kama ambavyo tulitegemea, yaani ulichofanya ni kuondoa maneno ya Muziki na kuweka ya Hasara Roho.

Kama msanii mkubwa, nilitegemea ungekuja na kitu tofauti kabisa, ambacho kingedh-ihirisha kuwa wewe ni mkali, lakini kitendo cha kukopi na kupesti, kimeonyesha udhaifu mkubwa.

Binafsi nilikutahadharisha kupitia ukurasa wangu wa Instagram kuwa baada ya Wimbo wa Muziki, ulikuwa na kibarua kikubwa sana cha kufanya wimbo mkali na mkubwa kuliko huo ili uendelea kusimama kwenye gemu, lakini pia kupanda levo za kimataifa.

Nilisema hivyo kwa sababu suala siyo kuimba, ishu ni kuimba vizuri na kuweza kusimama sehemu ulipo. Hata kama angekuwa ni msanii mwingine, kile nilichokisema kwako ndicho ningemwambia.

Darassa ulipaswa kuwa na muda mzuri wa kutafakari nini Watanzania wanakihitaji baada ya Muziki, ilikuwa ni muda wa kufanya utafiti ni wimbo wa mtindo upi ukiutoa utaweza kukuvusha hapo ulipo na kuufikisha muziki wako kimataifa.

Nilichojifunza wasanii wetu wana pupa, mna haraka ya kutaka kuonekana mmeachia kazi mpya mara kwa mara bila kuangalia nini kitafuata kwenye kazi hiyo kama haitafanya vizuri au lah.

Nimeamua kukuambia kwa sababu mimi pia nawasilisha maoni na ushauri wa mashabiki wako ambao hawawezi kukufikia kwa njia ya barua. Lakini pia nimeandika ujumbe huu ili kukukumbusha kuwa kila kitu ni mipango ya muda mfupi na mrefu.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Muandishi umeongea maneno ya busara sana....kiherehere cha kutoa nyimbo mpya ndio kimemfanya kucopy na kupaste.
    Darassa ulitakiwa ukae na kutafakari ni muziki gani watu wanapenda kwa sasa, naikubali ngoma yako ya '' This is too much'' lakini kwa hii umechemsha ndugu!
    Maneno mazuri ya ''Hasara roho' lakini beat ileile ya Muziki...basi ndugu yangu na wewe unataka kuwa kama kina Snura kwa kukurupuka na ngoma zake zote zinafanana.

    Nawakilisha.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad