EVERTON ya Uingereza Yaingia Mkataba na Mdhamini wa Simba Sc ya Tanzania..!!!


SIKU chache baada ya Kampuni ya SportPesa kutangaza kuidhamini klabu ya Simba kwa mkataba wa miaka mitano wenye thamani Sh. bilioni 4.9, kampuni hiyo imeimarisha uwapo wake katika soko barani Ulaya baada ya Jumatatu kukubali kuwa mshirika mkuu wa klabu ya Everton ya England.

Dili hilo kwa Everton ambayo imekuwa mshindi mara tisa (9) England, limeanza rasmi Jumatatu na jezi mpya zenye kuitangaza SportPesa zitaanza kutumika kuanzia msimu wa 2017/18.

Wakizungumza katika uzinduzi wa dili hilo kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Liverpool, Mkurugenzi Mkuu wa klabu ya Everton, Robert Elstone, alisifia makubaliano hayo ya kihistoria.

“Tunaikaribisha SportPesa kwenye familia ya Everton na tunatazamia kufanya kazi kwa ukaribu na kampuni hiyo ambayo inakua kwa kasi duniani.

Tangu kuanza kwa mazungumzo yetu, kwa pamoja tumekuwa tukivutiwa na mlingano wa maadili na malengo ya SportPesa ambayo yanawiana na yale ya klabu yetu.

Kwa miaka ijayo tutashirikiana kikamilifu katika kutimiza malengo yetu,” alisema.

Meneja masoko wa SportPesa Uingereza, Shaun Simmonds, alisisitiza uhusiano wao na Everton, kama moja ya taasisi zinazoheshimika katika ulimwengu wa soka kwani inaendana na mkakati wa kampuni katika kukuza michezo kwa kupanua wigo wake ndani ya Uingereza.

“Tunajisikia fahari, mafanikio ya SportPesa Uingereza na shughuli za SportPesa barani Ulaya kwa ujumla pamoja na ushirikiano ambao ushirika huu utaleta maendeleo katika shughuli zetu barani Afrika na ulimwenguni,” aliongeza Simmonds.

Kwa Tanzania, Kampuni ya SportPesa imeukaribisha ujio wa Everton katika udhamini ambao unaonesha dhamira ya kweli katika maendeleo ya mpira wa miguu.

“Ndiyo maana hapa Tanzania, Sportpesa imejiingiza katika udhamini kwa klabu za Tanzania, ikiwa ni kuungana na Sportpesa nchi nyingine kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu,” alisema Tarimba Abbas, Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa SportPesa Tanzania.

Kampuni ya SportPesa ilianza rasmi nchini Kenya mwaka 2014 na tangu hapo imekuwa ikikua kimataifa.

Kuongezeka kwa ushirika na klabu ya Everton ni hatua mpya katika kukuza orodha ya timu washirika ambapo timu hiyo kutoka Jiji la Liverpool itaungana na klabu za Hull City, Southampton, Arsenal [zote za England], Gor Mahia, AFC Leopards [Kenya] na Simba SC [Tanzania].

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad