Kauli ya mbunge huyo imekuja baada ya hivi karibuni kikao cha Baraza la Madiwani katika Jiji la Arusha kupitisha azimio la kodi za vibanda vilivyojengwa stendi ndogo mjini Arusha kutakiwa kulipia halmashauri moja kwa moja na si kupitia madalali.
Jana Lema alisema kwa muda mrefu kumekuwa na hali ya kutoheshimiwa kwa maazimio yanayotolewa na Baraza la Madiwani jambo ambalo halileti picha nzuri kwa jamii.
Alisema jiji liliingia mkataba wa miaka 10 na waliojenga vibanda hivyo tangu mwaka 1994 na baada ya hapo vitarudi chini ya umiliki wa halmashauri ya jiji lakini tangu wakati huo hadi sasa kumekuwa na kutoelewana na Serikali imekuwa ikikosa mapato yake.
“Tunajua huenda ni mkakati maalumu unaofanywa na Mkurugenzi wa Jiji (Athuman Kihamia) kupitia Mkuu wa Mkoa wa Arusha (Mrisho Gambo).
“Ni wazi huu ni mkakati wa kudhoofisha halmashauri ambazo zipo chini ya upinzani hasa Chadema ili zionekane zimeshindwa kusimamia rasilimali ikiwemo ukusanyaji wa mapato.
“Kutokana na hali hii ninamwomba sana Rais Dk. John Magufuli, kama aliweza kuunda tume na ikachunguza suala la mchanga wa dhahabu na akawafukuza kina Acacia basi afanye hivyo na kwa jiji la Arusha na kama itaonekana vinginevyo avunje Baraza la Madiwani nasi tutarudi mtaani na kuwa madiwania wa wananchi kuliko kutoheshimiwa maamuzi ya vikao.
“Mtu amejenga kibanda miguu mitatu kwa mitano tangu mwaka 1994 anakusanya kodi je hadi leo hajarudisha fedha zake? Kuna nini kinachoendelea na kwanini madiwani wanadharauliwa? Nakuombas Rais Magufuli tupia jicho lako Arusha,” alisema Lema
Mbunge huyo alikwenda mbali na kudai kwamba wapo baadhi ya viongozi wa Serikali wamekuwa wakiandaa mikakati kwa kushirikiana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yenye lengo la kudhofisha maeneo yanaongozwa na wapinzani.
“Tunaona wazi huu huenda ni mkakati wa kudhofisha upinzani kwani hata kauli ya CCM kupitia kwa Katibu Mwenezi wake, Humphrey Polepole kwamba viongozi wa Serikali kupelekwa kwenye maeneo ya upinzani. Kauli hii aliitoa akiwa Arusha na kilio chetu hiki tumekifikisha hadi kwa Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene naye anajua kila kitu,” alisema
Alisema suala la malipo hayo awali wafanyabiashara walikubaliana na uamuzi wa jiji lakini baada ya kuteuliwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Arusha ambaye kwa sasa ni mkuu wa mkoa, Mrisho Gambo aliingia suala hilo na kumpa maagizo kwa kuwakingia kifua watu waliojenga vibanda hivyo.