Nahodha Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, anaendelea na majaribio yake kwenye kikosi cha Randers FC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Denmark.
Himid tayari ameshafanya mazoezi mara kadaa mpaka sasa toka awasili ndani ya kikosi hiko cha Randers.
Kwa mujibu wa mtandao wa klabu hiyo, umeeleza kuwa kiungo huyo nyota mkabaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, 24, yuko tayari kwa mara ya kwanza kucheza soka la kulipwa na kulipa kisogo soka la nyumbani kwa kuhakikisha anapata mkataba wa kusajiliwa na Randers.
Nyota huyo ambaye atafanya majaribio ndani ya timu hiyo kwa siku 10, aliondoka nchini Jumatatu iliyopita baada ya pande zote mbili za timu hizo kufanya makubaliano kuhusu mchezaji huyo,
Mara baada ya kumaliza zoezi hilo atarejea mara moja Azam FC kabla ya taratibu nyingine kufuata kama watakuwa wamevutiwa na huduma yake.
Habari njema ni kuwa mbali na kufanya mazoezi na Randers, pia anatarajia kucheza mchezo mmoja akiwa na kikosi cha wachezaji wa akiba wa Randers kitakachocheza na AC Horsens Jumanne ijayo kwenye Ligi ya Wachezaji wa Akiba ndani ya Ligi Kuu ya Taifa hilo ‘Danish Superliga’.