HISTORIA :Hivi Ndivyo Nyerere Alivyomtetea Karume Mbele ya Viongozi wa Afrika Nchini Ghana..!!!


Na  AHMED RAJAB

KATIKA mwezi wa Machi hali ya hewa jijini Accra, Ghana, huwa inaudhi bila ya kiasi kwa joto linavyokuwa kali. Jioni ndipo huzidi kushtadi.  Nadra mvua kunyesha.  

Siku moja Machi 1958, saa za Magharibi, wakombozi wawili wa Kiafrika walikaa, glasi mkononi, wakipunga upepo kwenye baraza ya hoteli ya Avenada, iliyokuwa ikimilikiwa na Mgiriki.

Upande mmoja alikuwa Sheikh Ali Muhsin Barwani kutoka Zanzibar na aliyemkabili alikuwa Mwalimu Julius Nyerere kutoka Tanganyika.  Nyerere alikuwa rais wa chama kikuu cha Tanganyika cha kupigania uhuru, Tanganyika African National Union (TANU) na Barwani, akitambulika kuwa kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party (maarufu Hizbu) ingawa hakuwa na wadhifa maalum katika chama hicho. 

Rais wa Hizbu alikuwa Sheikh Vuai Kitoweo, mzawa wa Jambiani, kwenye mwambao wa kusini mashariki mwa Unguja. Kitoweo alishikilia wadhifa huo tangu alipochaguliwa 1955 hadi mapinduzi ya 1964.  Hata hivyo, Barwani ndiye aliyekuwa akionekana kiongozi wa Hizbu hata akapewa lakabu ya “zaimu”, inayotokana na neno la Kiarabu “zaim” lenye maana ya kiongozi.  

Wakati huo, Hizbu kilikuwa chama pekee kilichokuwa kikipigania uhuru wa Zanzibar. Chama kingine kikuu, cha Afro-Shirazi Party (ASP), kilikuwa kikipinga Zanzibar isipewe uhuru.  Ilifika hadi hata Waingereza walipokubali pafanywe uchaguzi Zanzibar, chama cha ASP kilipinga.  Uchaguzi huo ulikuwa wa  mwanzo katika Afrika ya Mashariki, ya Kati na kusini mwa Afrika, 

Sheikh Shaaban Soud Mponda, Mwafrika aliyekuwa mjumbe wa kuteuliwa katika Baraza la Kutunga Sheria (Legico) alihuzunika na kusema: “Hii ni siku ya giza kwa Waafrika wa nchi hii.”  Mponda akiunga mkono ASP. 

Mwafrika mwengine kwenye Baraza hilo, Sheikh Rashid Hamadi alimpinga akisema: “Sifahamu vipi katika karne hii ya maendeleo kuwa bado wapo watu wasiotaka uhuru. Haki ya mtu kumchagua mwakilishi wake ni hatua ya mwanzo ya kufikia uhuru.”  Hamadi, aliyetoka Ole, Pemba, alikuwa Hizbu.

Siku hizo kaulimbiu ya ASP ilikuwa: “zuwiya”, ikimaanisha uhuru wa Zanzibar uzuiwe.  Hoja ya ASP ilikuwa kwamba uhuru ukipatikana utawafaidia Waarabu waliokuwa wamepata elimu zaidi ya Waafrika.  

Chama cha ZNP (Hizbu) kiliundwa 1955 na miaka miwili baadaye Februari 5, 1957 Nyerere alisaidia kuasisiwa kwa ASP kwa kuziunganisha African Association na Shirazi Association, jumuiya ya Waafrika na ile ya Washirazi.  Chama hicho kilizaliwa kutoka tumbo la ukabila na hata ukunga wake ulikuwa wa kikabila. 

Mikono ya wakoloni wa Kiingereza pia ilionekana katika uzalishaji wa ASP. Hilo halikuwa jambo la kushangaza.  Waingereza walikwishazoea kufanya mambo kama hayo.  Hata Tanganyika mapema 1951, kabla ya TANU kuundwa, wakoloni walimwendea Abdulwahid Sykes na viongozi wenzake wa Tanganyika African Association (TAA), ambayo Nyerere alikuwa mwanachama wake, wakawaambia waunde chama cha siasa kitachokuwa na watu wa makabila mbalimbali.  

Sykes na wenzake walikataa kuwa vibaraka wa Waingereza. Waingereza wakamtomeza V.M. Nazerali, Mtanganyika mwenye asili ya Kihindi, na aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (Legico) amwandikie barua Dossa Aziz na kumshauri aunde chama cha aina hiyo. Aziz naye alikataa.

Viongozi kadha wa kadha, wakiwa pamoja na Watanganyika wenye asili ya Kihindi, waliendewa na Waingereza waunde chama wakitakacho wao lakini Waingereza waliondokea patupu. 

Kama miaka mitatu baadaye, baadhi ya viongozi hao waliigeuza TAA iwe TANU, chama cha ukombozi. Waliokata uamuzi huo muhimu walikuwa Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, John Rupia, Dossa Aziz na Julius Nyerere. Mwandishi Mohamed Said ameandika kwa urefu kuhusu historia hii na jinsi Nyerere alivyowapiku wenzake.

Walipokuwa kwenye baraza ya Hoteli Avenada, Barwani na Nyerere walikuwa wakinywa huku wakizungumzia mustakbali wa nchi zao.  

Barwani akinywa maji ya nanasi na Nyerere akipiga vitu vikali kidogo.  Barwani alimwambia Nyerere kwamba shida kubwa aliyokabiliana nayo ilikuwa uhaba wa skuli.

“Hatuna skuli za sekondari za kutosha na baada ya sekondari hatuna kitu,” alisema Barwani.

Kwa mujibu wa Barwani,  Nyerere alimjibu hivi: 

“Miye sihitaji elimu, si kwa sasa. Bahati yangu sina watu wengi waliosoma, kwani ni hao wachache (waliosoma) wanaonipa taabu. Watu kama Fundikira, Lugusha, Marealle, ndio wenye kunipinga. Sitaki wengine zaidi ya hao kwa sasa. Elimu itakuja baada ya uhuru.

“Ninachotaka ni magari ya aina ya Land Rover. Nchi yetu ni kubwa, kubwa sana. Ili tushinde uchaguzi ujao, itatubidi tufanye kampeni nchi nzima.  Nitafurahi sana nikipata nchi itayotupa magari ya Land Rover.”

Fundikira aliyemkusudia Nyerere alikuwa Abdallah Said Fundikira aliyekuwa Chifu wa Wanyamwezi wa Itetemya, Tabora.  Lugusha alikuwa Chifu Haroun Msabila Lugusha wa Wanyamwezi wa Sikonge, Tabora, na Marealle alikuwa Chifu Thomas Lenana Marealle, aliyekuwa Chifu Mkuu (au Mangi) wa Wachagga wa Marangu, Moshi. 

Tunaweza kuandika mengi kuhusu kila mmoja wa waungwana hawa waliokuwa wazalendo lakini tukifanya hivyo tunaweza tukapotea njia na tukatoka kwenye mada yetu.

Mazungumzo hayo baina ya Ali Muhsin Barwani na Julius Nyerere ameyadhukuru Barwani kwenye kitabu cha kumbukumbu zake kiitwacho “Conflicts and Harmony in Zanzibar”. 

Barwani na Nyerere walikuwa Accra wakihudhuria sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja tangu  Ghana iwe huru.  Walikuwa wageni wa Nkrumah. Waalikwa wengine walikuwa pamoja na Mallam Aminu Kano (Nigeria), Joseph Murumbi na Tom Mboya (Kenya), Rashidi Kawawa na Paul Bomani (Tanganyika), Kanyama Chiume (Malawi) na Eliradi Mulira (Uganda).  

Baada ya kumalizika shamrashamra za maadhimisho hayo, Nkrumah aliwaalika wageni wake nyumbani kwake.

Walipofika, Nkrumah aliwaambia kwamba alikuwa na siri aliyotaka kuwapa. Aliwaeleza kwamba aliwaalika katika sherehe za maadhimisho ya uhuru kama kisingizio kwa sababu akihofia ya kwamba angeliwaambia na mapema sababu hasa ya kuwaalika Ghana, pengine watawala wa kikoloni wangeliwazuia wasisafiri kwenda Accra.

Nkrumah alikuwa na George Padmore, mzawa wa Trinidad, mwandishi na mwanamajumui wa Kiafrika (Pan Africanist) aliyekuwa mshauri wake mkuu wa mambo ya Afrika. Aliwaambia wageni wake kwamba sababu hasa iliyomfanya awaalike Accra ni kuwataka wajadiliane uwezekano wa kuratibu harakati za kuikomboa kila ardhi ya Afrika iliyokuwa chini ya wakoloni.

Nkrumah na Padmore wakawaelezea mpango waliokuwa nao wa kuandaa mkutano mwishoni mwa mwaka huo wa 1958 hukohuko Accra kujadili utumizi wa mbinu za amani, kama zile za Mahatma Gandhi wa India, ili Afrika ijikomboe.

Murumbi, mpiganiaji uhuru kutoka Kenya ambaye siku hizo akiishi Uingereza kwa sababu wakoloni hawakumruhusu aishi Kenya, alisikiliza kwa makini.

Angekuwa Murumbi anaishi Zanzibar ya leo angeingizwa katika kaumu ya wanaoitwa “machotara” na  wabaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Angetiwa katika kundi hilo kwa sababu baba yake alikuwa Goa, kutoka India, na mamake alikuwa Mmasai. 

Kwa muda mrefu Murumbi alikuwa akisafiria paspoti ya Morocco aliyopewa na babu yake Mfalme Mohamed wa sasa. Alipokuwa London, Murumbi alifanya kazi kubwa ya kuueleza ulimwengu kuhusu madhila yaliyokuwa yakifanywa na wakoloni nchini Kenya.

Siku hiyo alipokuwa Accra nyumbani kwa Nkrumah akimsikiliza kiongozi huyo wa Ghana na mshauri wake Padmore, Murumbi alikuwa na swali lililokuwa likimhangaisha.

Aliuliza: “Tuwaalike viongozi wote, au wale tu tunaowajua kuwa ni wazalendo? Kwani kuna baadhi ya viongozi kama vile wale wa Afro-Shirazi wa Zanzibar wenye kukipinga chama cha Ali Muhsin, na wanajulikana kuwa ni vibaraka wa Waingereza. Tuwaalike nao pia?”

Nkrumah, aliyekuwa amekaa kitini, nusura aruke. Alifoka: “Hapana! Hatuwezi kuwa nao vibaraka!”

Nyerere aliingilia kati kumsaidia rafiki yake kiongozi wa ASP, chama ambacho yeye mwenyewe alisaidia kukiunda.

Alisema: “Nadhani itakuwa jambo la busara zaidi kuwaalika. Watu kama hao si vibaraka kwa imani. Hawajui (mambo). Wakija hapa na kuwa nasi watashajiika kuwa na msimamo wa kizalendo, na hivyo wataiimarisha dhamira yetu badala ya kuidhoifisha.”

Nyerere aliitoa hoja yake kwa ulimi wa asali. Na ilikuwa vigumu wenzake kumpinga. Padmore akatoa rai ya namna ya kulitanzua tatizo hilo.

“Tutauandika mwaliko kwa namna ambayo wakikubali kuja, mabwana zao wa kikoloni hawatokuwa tena na imani nao, na watajikuta peke yao,” alisema Padmore.

Taarifa ya mwaliko wa mkutano huo wa mwisho wa mwaka wa 1958 iliulaani vikali ukabila.  Kwa vile ukabila ulikuwa moja ya nguzo za ASP, kama ilivyotazamiwa Karume aliupinga mkutano wa Accra.

Alipopelekewa mwaliko alifanya mkutano mkuu wa hadhara Miembeni, Unguja, na akasema: “Uhuru wetu hautotoka Accra, wala hautotoka Cairo. Utapokuja, utatoka London. Wenye kudai uhuru sasa ni wapumbavu. Hatuwezi hata kutengeneza sindano.  Bado tuna miaka mingi ya kujifunza kutoka kwa Waingereza. Tutapokuwa tumekwishajifunza ndipo tutapowaambia waalimu wetu ‘Goodbye’. Sendi popote kutafuta uhuru.”

Karume aligoma.  Hakutaka kwenda Accra kuhudhuria Mkutano wa Mwanzo wa Waafrika Wote (All African People’s Conference).  

Vuguvugu la Umajumui wa Kiafrika la Afrika ya Mashariki na ya Kati (PAFMECA) liliwatuma Francis Khamisi kutoka Kenya na Kanyama Chiume kutoka Malawi kwenda Zanzibar kusema naye Karume.  Baada ya kumbembeleza kwa muda mrefu, hatimaye Karume akakubali kwenda Accra akifuatana na Barwani pamoja na Abdulrahman Babu aliyekuwa katibu mkuu wa Hizbu.

Hatujui pangetokea nini Nyerere angelishindwa kumtetea Karume mbele ya Nkrumah.  Gurudumu la historia likishapitia njia fulani huwa muhali, haiwezekani kabisa, kulirejesha nyuma na kulifanya lipite njia nyingine. Likishapita ndo limekwishapita. 

Lile la historia ya Zanzibar tangu mwongo wa 1950, kwa kiwango kikubwa, limekuwa likisukumwa na Nyerere.  

Tangu aanze kuziingilia siasa za Zanzibar 1957, Nyerere ndiye aliyekuwa akilisukuma gurudumu hilo .  Alifanya hivyo kwanza kwa kuzishawishi siasa za ASP na baada ya Aprili 1964 kwa kuidhibiti Zanzibar nzima.  Gurudumu alilolisukuma ndilo lililoifikisha Zanzibar hapa ilipo.a

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad