Wakati akitimiza takriban siku 572 akiwa Ikulu, Rais John Magufuli anaonekana bado hajapata timu sahihi inayoendana na falsafa yake ya utendaji kazi, akiendelea kupanga na kupangua viongozi na watendaji wa Serikali.
Kitendo cha kutengua uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo, mtu ambaye alitumia maneno mazuri mbele ya wananchi kuwaonyesha kuwa waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini ni mchapakazi na kumtaka ajitahmini, ni kati ya viashiria kuwa bado JPM anasaka timu sahihi.
Pia Rais alivunja bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), kumsimamisha mkurugenzi mkuu na kutaka wafanyakazi wa TMAA na wizara wachunguzwe, kinaonyesha bado Magufuli anaendelea kujenda timu ya “kuchapa kazi tu”.
Mbali na hilo, mkuu huyo wa nchi amekuwa na mtindo wa kuwapa watendaji nafasi za kukaimu, kama alivyofanya kwa Profesa Ibrahim Hamisi Juma, ambaye anakaimu nafasi ya Jaji Mkuu, jambo lililoibua mijadala.
Tayari Rais Magufuli ameshaacha mawaziri watatu tangu alipounda baraza lake mapema mwaka jana, wawili akiwa ametengua uteuzi wao na mmoja kumuacha katika mabadiliko madogo.
Uteuzi wa Charles Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Muhongo ulitenguliwa kwa makosa tofauti, wakati Nape Nnauye aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliachwa katika mabadiliko hayo madogo.
Pia, ameshabadilisha mawaziri kutoka wizara moja hadi nyingine katika kipindi kisichozidi miaka miwili tangu aapishwe Novemba 5 mwaka juzi.
Kwenye panga pangua hiyo ya watendaji, Rais Magufuli ameonekana ni mwiba mkali hadi kufikia hatua ya kuwaengua marafiki zake wa karibu aliowateua kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo uwaziri.
Tukio ambalo halikutegemewa ni la kutengua uteuzi wa Ernest Mangu, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na kumteua Simon Sirro kushika nafasi hiyo, akiahidi kumpangia kazi nyingine Mangu.
Hakuna sababu zilizotolewa za mabadiliko hayo, hivyo kuacha fursa ya ubashiri kuwa huenda kulitokana na kutosimamia vyema vitendo vya mauaji ya viongozi na askari wa Jeshi la Polisi katika wilaya tatu za mkoani Pwani.
“Ili kuongoza unatakiwa kuwa na watu au wasaidizi wenye maono sawa na wewe,” alisema mhadhiri wa Idara ya Sayansi Asilia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Frank Tily.
“Baada ya kuingia madarakani Rais alichagua baadhi ya watendaji akiamini kuwa watamsaidia, lakini mwisho wa siku wanaonekana wapo tofauti na maono ya mkuu.”
Alisema kwa mamlaka aliyokuwa nayo, Rais ana haki ya kutengua na kuteua mtendaji anayeona anafaa na kuhakikisha malengo yao yanafanana ili kuwatumikia vyema Watanzania.
“Anaisuka Serikali iwe safi, ili afikie malengo yake. Mwanzo wakati wa kuingia madarakani hakuwajua vizuri baadhi ya watendaji,” alisema Dk Tily.
Maoni kama hayo yalitolewa na mhadhiri mstaafu wa UDSM, Dk Ahmed Kiwanuka aliyesema Rais Magufuli ana nia njema na Taifa hili, pia ana wajibu wa kisheria na madaraka ya kuwapima watendaji kwa kutumia vigezo vyake.
“Ni wajibu wake kutekeleza majukumu haya. Ukiwa nje huwezi kujua ugumu anaoupata wakati wa kutekeleza majukumu yake,” alisema Dk Kiwanuka.
Alisema kufanikiwa kwa Rais Magufuli ni mafanikio ya Taifa na Watanzania kwa ujumla hivyo aungwe mkono katika jitihada zake za kuleta maendeleo.
Naye mhadhiri wa Idara ya Siasa, Sayansi na Utawala ya Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alisema kiongozi hawezi kufanya peke yake, bali huwa na timu na pale anapoona kuna kinachomkwamisha, anaweza kufanya mabadiliko.
“Serikali siyo klabu ya karata au watu kucheza bao kwa hiyo hata rafiki kama hafanyi kazi vizuri, unaweza kumuondoa,” alisema.
Alisema mwaka 2020 ni wa uchaguzi na wananchi watamuuliza kama alitimiza malengo yake alipokuwa madarakani.
Mhadhiri huyo alisema, hata hivyo, kuwa panga pangua hiyo ina athari zake kwa kuwa kiongozi hakai muda mrefu sehemu moja na hivyo anashindwa kujifunza au kupanga mipango yake ya maendeleo.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ameonyesha kutostahimili viongozi wanaokwenda kinyume na sera zake, akiwatimua baadhi kwa kutofuata maagizo yake, kutowajibika ipasavyo katika masuala muhimu kama ukwepaji kodi bandarini, kukiuka maadili na kutuhumiwa kwa ufisadi.
Panga pangua hiyo iliondoa hadi watu aliowatangaza hadharani kuwa marafiki zake, kama Kitwanga, mbunge wa Misungwi (CCM) aliyetenguliwa kwa kuingia bungeni akiwa amelewa.
Kabla ya kutenguliwa, Kitwanga alikuwa akizongwa na wabunge kumtaka ajiuzulu akituhumiwa kuwa na hisa katika kampuni iliyohusika katika mkataba wa Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi ambao haukutekelezwa ipasavyo.
Nafasi ya Kitwanga ilichukuliwa na Mwigulu Nchemba aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Uvuvi, kisha Rais Magufuli alimteua Dk Charles Tizeba kuziba nafasi ya Nchemba.
Mbali na hao, Rais Magufuli alimuacha Nape katika mabadiliko madogo yaliyofanyika siku moja baada ya mbunge huyo wa Mtama (CCM) kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda ya kuchunguza uvamizi wa studio za televisheni za Clouds Media, huku mteule wa Rais akituhumiwa kuongoza tukio hilo.
Rais hakutaja sababu za kumuacha Nape badala yake katika mabadiliko hayo alimteua Dk Harrison Mwakyembe kushika nafasi yake huku Profesa Palamagamba Kabudi akiteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Diwani Athuman atenguliwa
Mbali na uteuzi wa Kamanda Sirro kuwa IGP, Rais Magufuli pia alimuondoa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman na baadaye kumteua kuwa katibu tawala wa Mkoa wa Kagera.
Taarifa ya Ikulu haikueleza sababu za kutenguliwa kwa Diwani, lakini ilikuwa ni siku moja baada ya Rais kutembelea ofisi za Idara ya Maliasili kuthibitisha shehena ya pembe za ndovu zilizokamatwa na kuhoji sababu za mtu anayeitwa Mpemba kuwasumbua polisi.
Nafasi yake ilichukuliwa na Robert Boaz, aliyekuwa kamishna wa polisi.
Rais pia amekuwa akifanya mabadiliko katika taasisi nyingine nyeti ya Mamlaka ya Mapato, akiwa ameshafanya mabadiliko mara tatu katika nafasi ya kamishna mkuu.
Mara alipoingia alimteua Dk Philip Mpango kuongoza taasisi hiyo, lakini baadaye akamteua kuwa mbunge na kumfanya awe Waziri wa Fedha na Mipango. Nafasi yake ikachukuliwa na Alphayo Kidata, aliyekuwa akikaimu nafasi ya kamishna msaidizi.
Ndani ya kipindi hicho kifupi, Rais Magufuli alimbadilisha tena Kidata na kumpeleka Ikulu, huku akimteua Charles Kichele kuongoza mamlaka hiyo muhimu.
Taasisi nyingine muhimu ni Takukuru, ambako alimuondoa mkurugenzi wa zamani, Dk Edward Hoseah kwa kutowajibika ipasavyo katika masuala ya ukwepaji kodi na ushuru wa makontena bandarini.
Badala yake, alimteua Valentino Mlowola kukaimu nafasi hiyo na baadaye kumthibitisha kuwa mkurugenzi mpya.
Hatua kama hiyo aliichukua kwa mkurugenzi wa Tanesco, Felschemi Mramba baada ya taasisi yake kuwasilisha maombi ya kutaka bei ya umeme iongezwe.
Rais pia alifanya mabadiliko katika shirika kubwa la Hifadhi ya jamii (NSSF) kwa kumuondoa Dk Ramadhan Dau kwa kumteua kuwa balozi, katika kipindi ambacho shirika hilo lilikuwa linamulikwa na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG).
Mwiba huo wa Rais Magufuli haukuacha kuwagusa pia, wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala na wakurugenzi.
Anne Kilango Malecela, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, alitenguliwa kwa kosa la kusema uongo kuhusu idadi ya watumishi hewa katika mkoa wake.
Credit - Mwananchi