KUNG’OLEWEA kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospter Muhongo, kumeibua upya mjadala juu ya sababu za kutodumu kwa kila anayeteuliwa kuongoza wizara hiyo katika miaka ya hivi karibuni.
Aidha, baadhi ya wabunge na wafuatiliaji wa masuala ya siasa wametaja sababu tano kuwa ndizo chanzo cha kutodumu kwa mawaziri wanaoshika wizara hiyo, ikiwamo ya kuwapo kwa mikataba ya fedha nyingi zaidi kuliko iliyoko katika wizara zingine.
Vyanzo vingine vinavyolinganishwa na zimwi linalowang’oa mawaziri kila uchao katika wizara hiyo vinatajwa kuwa ni changamoto za mianya inayosababishwa na baadhi ya vipengele vya Sheria ya Madini ya mwaka 2010; kukosekana uzalendo kwa baadhi ya watendaji katika wizara ambao mwishowe huwaponza mawaziri husika; kuwapo kwa mikataba iliyojaa utata na uelewa mdogo wa baadhi ya watendaji katika kuwashauri mawaziri husika juu ya masuala mbalimbali ya mikataba ya nishati na madini.
Muhongo aliyekuwa akiiongoza Wizara ya Nishati na Madini kwa mara ya pili baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya tano, aliondoshwa katika nafasi hiyo juzi kutokana na ripoti ya kamati teule ya Rais iliyochunguza usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) kwenda ughaibuni kubaini upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali, hali inayotokana na kuwasilishwa kwa taarifa potofu juu ya kila kilichomo kwenye makontena 277 ya mchanga huo yanayoshikiliwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Kabla ya Muhongo, wengine waliowahi kuongoza wizara hiyo katika kipindi cha kuanzia Serikali ya awamu ya nne ni Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, William Ngeleja, Muhongo, George Simbachawene na Muhongo aliyeongoza kwa mara ya pili, kuanzia mwaka 2016 hadi juzi.
KILICHOTOKEA KWA WALIONG’OKA
Wakati akipokea ripoti ya mchanga wa madini na kutangaza kumng’oa Muhongo juzi, Rais Magufuli alisema kutokana na kile kilichobainika, hana namna nyingine isipokuwa na kumwondoa licha ya kumpenda sana, tena ni rafiki yake.
“Ninampenda sana Profesa Muhongo, pia ni rafiki yangu… lakini kwenye hili ajifikirie, aji-asses (ajitathmini) na bila kuchelewa nilitaka aachie madaraka,” alisema kabla ya uamuzi kamili wa kutenguliwa nafasi yake kutolewa baadaye.
Pia nakala ya barua ya Muhongo kuachia ngazi ilionekana kwenye mitandao ya kijamii, ikimnukuu akisema ameamua kujiuzulu kutokana na ripoti ya Kamati Teule ya Rais kuhusu usafirishaji mchanga wa dhahabu.
Aliyeanza kuongoza wizara hiyo katika awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete kuanzia mwaka 2005 ni Dk. Msabaha. Hakudumu sana baada ya kuondolewa Oktoba, 2006 na kuhamishiwa katika Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Aliyefuatia baada ya Msabaha ni Nazir Karamagi. Naye hakudumu baada ya hatima yake kufika Februari 6, 2008 alipojiuzulu kutokana na matokeo ya ripoti ya Kamati ya Bunge iliyochunguza kashfa ya mkataba wenye utata wa Serikali kupitia Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni ya Richmond kwa ajili ya kufua umeme wa dharura.
Ripoti ya Bunge iliyomng’oa Karamagi na Msabaha pia ilisababisha Baraza la Mawaziri kuundwa upya baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu kutokana na ilibaini kuwa mchakato ulioipa Richmond zabuni ulighubikwa na vitendo vya ukiukwaji taratibu, kanuni na sheria za nchi.
Ngeleja akatwaa kijiti cha kuongoza wizara hiyo baada ya kuteuliwa na Rais Kikwete katika baraza jipya la mawaziri lililoundwa baada ya mtikisiko wa kashfa ya Richmond.
Ngeleja naye aling’olewa Mei 2012 baada ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko makubwa ya baraza lake la mawaziri yaliyotokana na kishindo cha Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyofichua madudu mengi yaliyofanywa na wizara hiyo chini ya uongozi wake.
Ni hapo ndipo Rais Kikwete alipomteua Prof. Muhongo kuongoza wizara hiyo kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, zimwi linalong’oa mawaziri katika wizara hiyo halikumwacha Muhongo adumu. Rais Kikwete alilazimika kukubali kuondoka kwa waziri huyo baada ya wabunge kumhusisha katika kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Baada ya Muhongo kung’oka, Rais Kikwete alimteua George Simbachawene kushika nafasi hiyo, ambaye aliitumikia vyema hadi serikali ya awamu ya nne ilipomaliza muda wake wa kuwa madarakani mwaka 2015.
Kwa mara nyingine, Muhongo alirejea kuiongoza wizara hiyo baada ya Rais Magufuli kumteua katika baraza lake la mawaziri la Serikali ya awamu ya tano.
Hata hivyo, Muhongo alijikuta akikumbwa tena na mikasa ya kung’olewa mapema kwa mawaziri katika wizara hiyo juzi kutokana na kashfa ya mchanga wa dhahabu, ikiwa ni mara ya pili kwake kukutwa na masahibu hayo.
Credit - Nipashe,